Ticker

6/recent/ticker-posts

TAASISI ZA UMMA ZATAKIWA KUACHANA NA UTENDAJI WA MAZOEA ILI KUFANIKISHA DIRA 2050


Na Mwandishi Wetu - Pwani. 

Serikali imezitaka Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali kuachana na utendaji wa mazoea na kujielekeza katika uongozi unaozingatia matokeo, ubunifu, uwajibikaji na ushirikiano wa karibu na sekta binafsi ili kuharakisha utekelezaji wa DIRA ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Wito huo ulitolewa Jumanne jioni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, wakati akifungua Mafunzo Elekezi kwa Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali yanayoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Taasisi ya UONGOZI katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.


Mafunzo hayo ya siku nne yanafanyika chini ya kaulimbiu "Kutoka Maono mpaka Matokeo: Kufungamanisha Utendaji wa Mashirika ya Umma na DIRA 2050." 

Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Mkumbo alisema Tanzania imeweka lengo la kufikia uchumi wa kati wa juu na kukuza Pato la Taifa (GDP) kutoka dola za Marekani bilioni 85 hadi dola trilioni 1 ifikapo mwaka 2050 kupitia DIRA 2050.

Alisema mafanikio ya DIRA hiyo hayatategemea ubora wa sera na mipango iliyoandaliwa pekee, bali uwezo wa viongozi wa Taasisi za Umma kutafsiri maono hayo kuwa matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi.

“Jukumu mlilonalo ni kubwa. Tunahitaji viongozi wenye maono, uwajibikaji, ubunifu na uadilifu watakaoweza kutafsiri DIRA 2050 kuwa matokeo yanayopimika,” alisema.

Prof. Mkumbo alisema dunia ya sasa inabadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia, ushindani wa kimataifa wa kuvutia uwekezaji, mabadiliko ya tabianchi na mabadiliko ya masoko ya dunia, hivyo Taasisi za Umma hazina budi kubadilika ili ziwe sehemu ya suluhisho la changamoto za maendeleo.

Alisisitiza kuwa Serikali haitapima mafanikio ya taasisi kwa idadi ya vikao vinavyofanyika au taarifa zinazoandaliwa, bali kwa matokeo yanayopatikana kupitia utoaji wa huduma bora, ongezeko la tija, uwekezaji, ajira na mapato ya Serikali.

Aidha, aliwataka Watendaji Wakuu kuhakikisha mipango ya kimkakati ya taasisi zao, bajeti, mipango ya mwaka, mikataba ya utendaji na viashiria vya utendaji vinaendana na DIRA 2050 ili kila taasisi iwe na mchango unaopimika katika utekelezaji wa malengo ya Taifa.

Alisema DIRA hiyo imebainisha sekta za kimageuzi zitakazochochea ukuaji wa uchumi, zikiwemo kilimo, viwanda, utalii, ujenzi, madini, uchumi wa buluu, michezo na ubunifu, huduma za kifedha pamoja na sekta ya huduma, huku Taasisi za Umma zikipewa jukumu la kuwezesha ukuaji wa sekta hizo.

Prof. Mkumbo alisema utekelezaji wa DIRA 2050 unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi, wananchi na wadau wa maendeleo.

Alieleza kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya uwekezaji, ubunifu, uzalishaji na uundaji wa ajira, hivyo Taasisi za Umma zinapaswa kujiona si wadhibiti wa maendeleo pekee, bali pia wawezeshaji wa uwekezaji kwa kuweka mazingira rafiki ya biashara na kuvutia mitaji.

“Tunapaswa kujenga mazingira yatakayowezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa DIRA 2050. Ushirikiano huo ndio utakaoharakisha ukuaji wa uchumi na kufikia malengo ya Taifa,” alisema huku akionya taasisi za umma kutokuwa kikwazo kwa wawekezaji.


Aliongeza: “Ninyi mmepewa dhamana ya kuongoza mageuzi ya Taasisi za Umma. Watanzania wanatarajia kuona matokeo kupitia uongozi wenu. Fanyeni kazi kwa bidii, uadilifu na ubunifu ili taasisi mnazoziongoza ziwe chachu ya kufanikisha DIRA ya Taifa ya Maendeleo 2050.”

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema kaulimbiu ya mwaka huu inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha DIRA ya Taifa ya Maendeleo 2050 haitabaki kuwa maono ya muda mrefu, bali inageuzwa kuwa matokeo yanayopimika kupitia utendaji wa Taasisi za Umma.

“Hatutaifikia Tanzania tunayoitamani kwa kutegemea sera pekee. Tunahitaji taasisi zenye viongozi wanaoweza kutafsiri maono ya Taifa kuwa matokeo yanayopimika katika kila sekta,” alisema.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Dk. Fred Msemwa, alisema Watendaji Wakuu wana wajibu wa kuhakikisha taasisi wanazoongoza zinakuwa chachu ya kuvutia uwekezaji, kuongeza ushindani wa uchumi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Alisisitiza kuwa uongozi wenye maono, unaozingatia uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali za umma ni nguzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuharakisha maendeleo endelevu ya nchi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi, alisema mafunzo hayo ya siku nne ni sehemu ya utekelezaji wa sera za maendeleo ya rasilimali watu na uongozi katika Utumishi wa Umma, yakilenga kuwawezesha Watendaji Wakuu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Alisema matarajio ya Serikali ni kwamba maarifa na ujuzi watakaoupata washiriki kupitia mafunzo hayo yataakisiwa katika utendaji wao wa kila siku, hivyo kuimarisha ufanisi wa taasisi wanazoongoza na kuchangia kwa kiwango kikubwa kufanikisha utekelezaji wa Dira 2050.

“Matarajio yetu ni kuwa maarifa na ujuzi mtakaoupata kupitia mafunzo haya vitaonekana katika utendaji wenu wa kila siku na hatimaye kuchangia kwa kiwango kikubwa kufanikisha utekelezaji wa Dira 2050,” alisisitiza Bw. Mkomi.

Akihitimisha, aliwataka washiriki kuwasilisha mapendekezo kuhusu mahitaji ya rasilimali watu yatakayowezesha taasisi wanazoongoza kuwa chachu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa mujibu wa Msajili wa Hazina, ndiyo sababu Ofisi ya Msajili wa Hazina, kwa kushirikiana na Taasisi ya UONGOZI, imeendelea kuwekeza katika maendeleo ya uongozi kupitia mafunzo elekezi kwa Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali.

Alisema tangu programu hiyo ilipoanzishwa mwaka 2024, zaidi ya Watendaji Wakuu 187 wamepatiwa mafunzo hayo, huku viongozi wapatao 57 wakishiriki katika awamu ya mwaka huu.

Bw. Mchechu alisema mafunzo hayo yanawajengea viongozi uelewa wa matarajio ya Serikali, utawala bora, uwajibikaji, usimamizi wa uwekezaji wa umma, matumizi bora ya rasilimali na uongozi unaozingatia matokeo.

Alisema uwekezaji huo katika maendeleo ya viongozi tayari umeanza kuleta matokeo chanya, ambapo makusanyo ya gawio na michango yameongezeka kutoka Sh637 bilioni mwaka wa fedha 2020/21 hadi Sh1.327 trilioni mwaka 2025/26, sawa na ongezeko la asilimia 108.

“Matokeo haya yanaonesha kuwa uwekezaji katika uongozi ni uwekezaji katika uchumi wa Taifa. Kadiri tunavyojenga viongozi wenye uwezo, ndivyo tunavyojenga taasisi zenye tija na kuongeza mchango wake katika mapato ya Serikali,” alisema.

Alisema katika kipindi cha utekelezaji wa DIRA 2050, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeainisha maeneo matano ya kimkakati yatakayoongoza mageuzi ya Taasisi za Umma.

Maeneo hayo ni kuimarisha utawala bora, kuendeleza uongozi na rasilimali watu, kuimarisha usimamizi wa utendaji unaotegemea viashiria na ushahidi, kuwezesha upatikanaji wa rasilimali kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), masoko ya mitaji na mifuko ya uwekezaji, pamoja na kuongeza tija, faida na thamani ya uwekezaji wa Serikali.

Aliongeza kuwa mafanikio ya maeneo hayo yanategemea pia ushirikiano wa karibu kati ya Taasisi za Umma na sekta binafsi, ili kuongeza uwekezaji, matumizi ya teknolojia, ubunifu, ushindani wa uchumi na ajira.

Naye Bw. Kadari Singo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, alisema kuwa mafanikio ya utekelezaji wa Dira 2050 yatategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa mfumo imara wa uongozi.

Alisema ni muhimu kujenga mifumo ya kutambua na kuendeleza vipaji vya uongozi, kuhakikisha viongozi wanawekwa katika nafasi zinazolingana na uwezo wao, kuweka mipaka ya wazi ya mamlaka na majukumu yao, pamoja na kuimarisha uwajibikaji katika ngazi zote za uongozi.

"Masuala haya yanapaswa kupewa kipaumbele na kuzingatiwa kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050," alisema.

Katika mafunzo hayo ya siku nne, washiriki watapata mada kuhusu afya na ustawi wa viongozi, kufungamanisha mipango ya taasisi na DIRA 2050, uongozi wa kimkakati, usimamizi wa migogoro, usimamizi wa uwekezaji wa Serikali, utawala bora, usimamizi wa vihatarishi, ESG, fedha, ukaguzi pamoja na zoezi la kuandaa ahadi binafsi za utekelezaji wa DIRA 2050.

Post a Comment

0 Comments