Ticker

6/recent/ticker-posts

TANZANIA NI SALAMA, TUKO TAYARI KWA AFCON 2026 – KATAMBI

 



Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas Katambi, amesema Tanzania iko salama na imejipanga kikamilifu kuhakikisha mashindano ya AFCON 2026 yanafanyika katika mazingira ya amani, utulivu na usalama wa hali ya juu.

Katambi ameyasema hayo akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa katika vyombo vya ulinzi na usalama kupitia utoaji wa mafunzo ya weledi, ununuzi wa vitendea kazi vya kisasa pamoja na matumizi ya mbinu mpya za ulinzi wa kidijitali.

Amesema Tanzania imejipanga kwa kutumia mbinu na mikakati maalumu ya kiusalama, ikiwemo mikakati 30 ya ndani na nje ya nchi, ambapo 15 ni ya wazi na 15 ni ya siri, kwa lengo la kuhakikisha usalama wa taifa na mafanikio ya mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika.

Katambi amesema Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inaendelea kujidhatiti kimkakati, kimedani na kiteknolojia ili kuhakikisha AFCON 2026 inafanyika kwa usalama mkubwa, huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiendelea kuimarisha ulinzi katika viwanja vya michezo, maeneo ya mazoezi, hoteli za timu, viwanja vya ndege na sehemu zote za mikusanyiko ya mashabiki.

 Aidha, kutakuwa na ukaguzi maalumu katika njia za kuingia na kutoka kwenye maeneo yote ya mashindano ili kuimarisha usalama wa washiriki na watazamaji.
Ameeleza kuwa Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kusimamia umati wa watu kwa kuzuia msongamano, vurugu na matukio ya kukanyagana, sambamba na kutenga njia za dharura na maeneo salama kwa watazamaji.

 Pia kutaimarishwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Sekta ya Afya, Mamlaka za Serikali za Mitaa, waandaaji wa mashindano na kamati mbalimbali husika ili kuhakikisha operesheni zote za usalama zinafanyika kwa ufanisi.

Kwa mujibu wa Katambi, vyombo vya usalama vitaendelea kutumia mifumo ya kisasa ya ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za kiintelijensia ili kubaini mapema wahalifu, mienendo shuku na vitisho vinavyoweza kujitokeza, ikiwemo ugaidi, wizi, vurugu za mashabiki na uhalifu wa mtandaoni. 

Aidha, vitatumia mbinu mpya za kuzuia matukio kabla hayajatokea pamoja na teknolojia mbalimbali kama kamera za ulinzi (CCTV), mifumo ya utambuzi wa wahusika, vifaa vya mawasiliano na mifumo ya ufuatiliaji ili kuongeza ufanisi wa operesheni za kiusalama.
Katambi amesema Serikali pia imejipanga kuhakikisha usalama wa wachezaji, waamuzi, viongozi wa CAF, wageni wa heshima na mashabiki kutoka ndani na nje ya nchi kwa kuwapatia ulinzi wa kutosha na kuhakikisha usafiri wao unakuwa salama wakati wote. 

Vilevile, hatua kali zitachukuliwa dhidi ya vitendo vya wizi, ulanguzi wa tiketi, biashara haramu, matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vingine vinavyoweza kuvuruga mashindano.

Ameongeza kuwa Serikali imeandaa mipango ya kukabiliana na moto, majanga ya asili, dharura za kiafya na matukio mengine yasiyotegemewa, huku vikosi vya uokoaji na huduma za kwanza vikisambazwa katika kila eneo la mashindano. 
Sambamba na hilo, mashabiki wataendelea kuelimishwa kuhusu sheria za viwanjani, umuhimu wa kudumisha amani na wajibu wao wa kutoa taarifa za matukio ya kiusalama, pamoja na kuhamasishwa kushirikiana na vyombo vya dola.

Katambi amesema pamoja na hatua hizo zote, Tanzania itazingatia miongozo ya CAF na viwango vya kimataifa vya usalama wa matukio makubwa ya michezo. 

Amesema pia itatumia uzoefu na mikakati ya kiusalama aliyoipata wakati wa ziara yake nchini Marekani katika maandalizi ya Kombe la Dunia 2026, ikiwemo tathmini endelevu ya vihatarishi, uratibu wa taasisi mbalimbali na utekelezaji wa mipango ya dharura.

Amesema mafanikio ya usalama wa AFCON 2026 yatatokana na ushirikiano mkubwa kati ya vyombo vya dola chini ya usimamizi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, waandaaji wa mashindano, taasisi nyingine za Serikali, sekta binafsi na wananchi, ili kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika katika mazingira ya amani, utulivu na usalama kwa washiriki na mashabiki wote.

Aidha, Katambi amewaomba Watanzania pamoja na jumuiya za kikanda na kimataifa kupuuza watu au vikundi vinavyoichafua Tanzania kupitia mitandao ya kijamii kwa maneno au maandishi kwa maslahi binafsi, akisema vitendo hivyo vina lengo la kuhujumu uchumi, maendeleo ya jamii na Taifa.


Post a Comment

0 Comments