Ticker

6/recent/ticker-posts

Tanzania Yapongezwa kwa Hatua za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi

Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi (kulia), akiwa na Kaimu Balozi wa Australia nchini Tanzania, Andrew Barnes, mara baada ya kufanya mazungumzo kuhusu kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, yaliyofanyika katika Ofisi ya Makamu wa Rais jijini Dar es Salaam, Julai 31, 2026.

**************

Serikali ya Tanzania imepongezwa kwa juhudi zake za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia utekelezaji wa sera, mikakati na programu mbalimbali zinazolenga kujenga ustahimilivu wa mazingira, uchumi na jamii.

Pongezi hizo zimetolewa na Kaimu Balozi wa Australia nchini Tanzania, Andrew Barnes, alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, katika Ofisi ya Makamu wa Rais jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Barnes amesema Tanzania imeendelea kuonesha uongozi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia utekelezaji wa hatua mbalimbali zinazolenga kuimarisha ustahimilivu wa mazingira na maendeleo endelevu.

Aidha, amepongeza ujenzi wa ukuta wa kinga katika eneo la Barabara ya Obama jijini Dar es Salaam, akieleza kuwa ni mfano wa utekelezaji wa hatua madhubuti za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Amesema mradi huo umechangia kuimarisha ustahimilivu wa miundombinu dhidi ya mmomonyoko wa fukwe na mawimbi ya bahari, hivyo kulinda maisha ya wananchi, mali zao na miundombinu muhimu ya kiuchumi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amesema Serikali imeendelea kuyapa kipaumbele masuala ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutokana na athari zake zinazozidi kuongezeka na kuathiri maisha ya wananchi pamoja na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Ameeleza kuwa mabadiliko ya tabianchi si suala la kisayansi pekee, bali pia yana athari kubwa katika uchumi, usalama wa chakula, afya, mazingira na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Dkt. Muyungi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuonesha uongozi katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi barani Afrika kwa kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika wa Nishati Safi ya Kupikia (African Union Champion for Clean Cooking Energy), sambamba na kuwa mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSCC).

Amesema pamoja na jitihada hizo, bado kuna changamoto ya upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza mipango ya muda mfupi na muda mrefu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika upatikanaji wa fedha na teknolojia ili kusaidia utekelezaji wa mipango ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Aidha, Dkt. Muyungi amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kushiriki kikamilifu katika majukwaa ya kimataifa yanayojadili masuala ya mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo Mkutano wa Maandalizi wa COP31 (Pre-COP31) utakaofanyika nchini Fiji, pamoja na Mkutano Maalum wa Viongozi utakaofanyika nchini Tuvalu, kabla ya kushiriki Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) utakaofanyika jijini Antalya, Uturuki.

Amesema ushiriki wa Tanzania katika mikutano hiyo utaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kubadilishana uzoefu na kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya utekelezaji wa ajenda za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, sambamba na kuendeleza juhudi za taifa katika kujenga uchumi unaostahimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Post a Comment

0 Comments