Ticker

6/recent/ticker-posts

TBS WATOA ELIMU YA VIWANGO KWA WAJASIRIAMALI MAONESHO YA SABASABA 2026.

  Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam. Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kuonyesha dhamira yake ya kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kutumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), ambapo mamia ya wajasiriamali wamejitokeza kupata elimu kuhusu viwango na taratibu za kupata Alama ya Ubora kwa bidhaa zao.

Akizungumza katika banda la TBS lililopo ndani ya Banda la Wizara ya Viwanda na Biashara, Afisa Uhusiano Mwandamizi wa TBS, Bi. Neema Mtemvu, amesema maonesho ya mwaka huu yamekuwa na mafanikio makubwa kwa shirika hilo, huku zaidi ya wajasiriamali 200 wametembelewa na kupatiwa elimu kuhusu umuhimu wa kuthibitisha ubora wa bidhaa zao.

Amesema kupitia maonesho hayo, TBS imefanikiwa kuzungumza na wajasiriamali kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu viwango, kusikiliza changamoto zinazowakabili katika uzalishaji na biashara, pamoja na kuwapa ushauri wa kitaalamu utakaowawezesha kuboresha bidhaa zao ili zikidhi matakwa ya soko la ndani na nje ya nchi.

Bi. Mtemvu ameeleza kuwa mwitikio wa wajasiriamali umekuwa mkubwa, ambapo baadhi yao tayari wameanza taratibu za kupata Alama ya Ubora, hatua inayodhihirisha kuongezeka kwa uelewa kuhusu umuhimu wa viwango katika kukuza biashara na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania.

Amesisitiza kuwa gharama za kupata Alama ya Ubora kwa wajasiriamali zimegharamiwa na Serikali, hivyo huduma hiyo hutolewa bila malipo kwa kundi hilo maalum. Hatua hiyo inalenga kuwapa fursa wazalishaji wadogo na wa kati kuongeza thamani ya bidhaa zao, kuimarisha ushindani na kufungua masoko mapya bila kikwazo cha gharama za uthibitishaji.

Kwa mujibu wa TBS, bidhaa yenye Alama ya Ubora huongeza imani kwa walaji kutokana na kuthibitishwa kuwa imekidhi viwango vinavyotakiwa vya ubora na usalama. Aidha, alama hiyo hufungua milango ya bidhaa za Kitanzania kuingia katika masoko ya kikanda na kimataifa, hivyo kuchochea ukuaji wa biashara na uchumi wa taifa.

Ushiriki wa TBS katika Maonesho ya Sabasaba unaendelea kudhihirisha dhamira ya shirika hilo ya kusogeza huduma karibu na wananchi, kutoa elimu kwa vitendo na kuwafikia wajasiriamali popote walipo. Kupitia huduma zinazotolewa moja kwa moja katika maonesho hayo, wananchi wanapata fursa ya kuuliza maswali, kupata ushauri wa kitaalamu na kuanza taratibu za huduma bila kulazimika kufika katika ofisi za TBS.

Kwa kuendelea kutoa elimu na huduma kwa ukaribu, TBS inaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinakuwa salama, zenye ubora na zenye uwezo wa kushindana katika soko la ndani na la kimataifa, sambamba na kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda na ujasiriamali.






Post a Comment

0 Comments