NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI wa Idara ya Elimu Mbadala na Elimu ya Watu Wazima Zanzibar, Mashavu Ahmada Fakih, ameipongeza Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha sekta ya elimu nchini, huku akiwataka wadau wa maendeleo na wananchi kuendelea kuchangia Mfuko wa Elimu ili kuongeza ubora wa elimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Akizungumza leo Julai 11, 2026 katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mashavu amesema TEA imeendelea kuwa mshirika muhimu wa Serikali katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki yake ya elimu bila kujali mahali anapoishi.
Amesema mamlaka hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha miundombinu ya elimu Tanzania Bara na Zanzibar kupitia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya shule pamoja na taasisi mbalimbali za elimu, hatua ambayo imeongeza mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia.
Amebainisha kuwa mchango wa TEA umekuwa muhimu zaidi katika kipindi ambacho Tanzania inaendelea kutekeleza mageuzi ya sekta ya elimu kupitia mtaala mpya unaolenga kujenga umahiri, maarifa na ujuzi kwa wanafunzi ili waweze kujitegemea na kuchangia maendeleo ya taifa.
Amesema uwekezaji unaofanywa na TEA katika sekta ya elimu unasaidia kuwaandaa vijana wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha pamoja na kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa nchi.
"Elimu ni haki ya kila mwananchi na ndiyo msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Kupitia elimu, wananchi hupata maarifa, ujuzi na uwezo wa kushiriki katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya uchumi," amesema
Aidha, amewataka wadau wa maendeleo, sekta binafsi, taasisi mbalimbali na Watanzania wote kuendelea kuunga mkono juhudi za TEA kwa kuchangia Mfuko wa Elimu, akieleza kuwa ushiriki wa wadau utasaidia kuongeza kasi ya uboreshaji wa miundombinu na huduma za elimu nchini.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, TEA na wadau wa maendeleo utawezesha taifa kuwa na mfumo wa elimu unaozalisha wahitimu wenye maarifa, ujuzi na uzalendo, ambao watakuwa nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo ya Tanzania.

0 Comments