Ticker

6/recent/ticker-posts

TIRDO YATOA TEKNOLOJIA YA KISASA YA UCHAKATAJI NGOZI KWA MIMEA

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Matumizi ya kemikali katika uchakataji wa ngozi yanatarajiwa kupungua kufuatia ubunifu wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) wa kubuni dawa ya asili inayotokana na mimea, teknolojia inayolenga kulinda mazingira, afya za watumiaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za ngozi za Tanzania katika masoko ya ndani na kimataifa.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia za Nguo na Ngozi wa TIRDO, Mhandisi na Mtafiti Yusufu Sampuli, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Julai 3, 2026.

Amesema TIRDO imeendelea kuwekeza katika utafiti na ubunifu wa teknolojia zinazotumia malighafi za asili, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira badala ya kemikali zinazoweza kuathiri afya za binadamu na mazingira.

Kwa mujibu wa Sampuli, mwelekeo wa dunia kwa sasa unasisitiza matumizi ya bidhaa zinazozingatia uhifadhi wa mazingira na afya, hali ambayo imeongeza mahitaji ya bidhaa zilizochakatwa kwa kutumia malighafi za asili, hususan katika masoko ya kimataifa.

“Wananchi wanapaswa kufahamu kuwa dunia inapambana kulinda mazingira na afya za wafanyakazi pamoja na watumiaji wa bidhaa mbalimbali. Hivi sasa soko la bidhaa zilizochakatwa kwa kutumia vitu vya asili limeongezeka kwa kiasi kikubwa. Ukitazama soko la Ulaya, kuna mahitaji makubwa ya ngozi zilizochakatwa kwa kutumia mimea kuliko zile zinazotumia kemikali ambazo zina madhara kwa afya na mazingira,” amesema Sampuli.

Amesema ubunifu huo tayari umeanza kuleta matokeo chanya, ambapo baadhi ya wajasiriamali wa mkoa wa Kilimanjaro wameanza kutumia dawa hiyo ya asili katika shughuli za uchakataji wa ngozi na kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko.

Aidha, amesema TIRDO inaendelea kuwafuatilia na kuwapa ushauri wa kitaalamu wajasiriamali hao ili kuhakikisha teknolojia hiyo inatumika kwa ufanisi, kuongeza thamani ya bidhaa za ngozi na kuzifanya ziwe na uwezo mkubwa wa kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Sampuli ametoa wito kwa wadau wa sekta ya ngozi, wajasiriamali na wananchi kutumia teknolojia hiyo ya asili ili kuongeza tija ya uzalishaji, kulinda mazingira na kuchangia maendeleo ya sekta ya viwanda nchini.

Ameongeza kuwa dawa hiyo ya asili inapatikana kupitia TIRDO, huku wananchi na wadau wakihimizwa kufika katika ofisi za shirika au kutumia njia zake rasmi za mawasiliano ili kupata taarifa zaidi kuhusu matumizi ya teknolojia hiyo na huduma nyingine za utafiti na maendeleo zinazotolewa na taasisi hiyo.

Post a Comment

0 Comments