Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imehitimisha kikao cha tathmini ya utendaji kazi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kilichodumu kwa siku 5 jijini Arusha na kuja na mikakati ya kukusanya Sh. Trilioni 41.830 ilizopangiwa na Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Akihitimisha kikao hicho Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA Bw. Uledi Abbas Mussa amesema ili kufikia malengo hayo ya makusanyo watumishi wa Mamlaka hiyo wanapaswa kuendeleza uhusiano mzuri uliopo baina yao na walipakodi.
Ameipongeza TRA kwa mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa majukumu yake ya ukusanyaji mapato na utoaji huduma kwa walipakodi na kueleza kuwa kuvunja rekodi ya makusanyo kwa TRA siyo ajali bali ni mikakati iliyowekwa na kufanyiwa kazi.
Amesema mafanikio hayo yanapaswa kuwa chachu ya kuongeza bidii zaidi ili kufikia malengo makubwa ya taasisi na Taifa kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa juhudi za pamoja na nidhamu ya kazi ni msingi muhimu wa kuendeleza mafanikio hayo na kueleza kuwa nchi mbalimbali zimekuwa zikijifunza kutoka kwa mifumo na mbinu zinazotumiwa na TRA katika ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda, amesema mikakati waliyoweka katika kikao hicho itawawezesha kukamilisha na kuvuka lengo la kukusanya sh. Trilioni 41.830.
Amesema kwa mujibu wa makusanyo ya kodi ya mwaka wa fedha ulioishia Juni 2026 ya Sh. Trilioni 37.96 ikiwa ni sawa na asilimia 105 ya lengo la kukusanya Sh. Trilioni 36.07 TRA ilifikia wastani wa kukusanya Sh. Trilioni 3.165 kwa mwezi lakini kwa lengo jipya walilopewa na Serikali watatakiwa kukusanya Sh. Trilioni 3.480 kwa mwezi.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kumekuwa na ongezeko la makusanyo ya Sh. Bilioni 320 kwa kila mwezi lengo ambali watalifanikisha kwa pamoja kwa kushirikiana na walipakodi wote kwa nhi nzima.
"Wakati Rais wa awamu ya sita anaingia madarakani TRA ilikuwa na uwezo wa kukusanya Sh. Trilioni 21 lakini hivi sasa uwe,o wake ni kukusanya Sh. Trilioni 41.830, hii ni hatua kubwa inayoashiria kukua kwa biashara na shughuli za uchumi nchini", amesema Mwenda.
Amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027 TRA itaendelea kuwezesha biashara kupitia Dawati maalumu la uwezeshaji Biashara nchini na kuwatembelea Walipakodi kwa lengo la kuwasikiliza na kutatua changamoto zao.
Kuhusu makadirio ya kodi amesema TRA itaendelea kutenda haki kwa kutoa makadirio ya kodi yanayowiana na kipato na hali ya biashara ya Mlipakodi husika.
Amewataka viongozi wa taasisi hiyo kuongeza juhudi katika kukuza mahusiano mema na walipakodi pamoja na kushughulikia kwa haraka changamoto zinazowakabili.
Amesema uhusiano mzuri kati ya TRA na walipakodi ni nguzo muhimu katika kufanikisha ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Kuhusu TRA United Kamishna Mkuu amewapongeza kwa kuwa Mabalozi wazuri wa kodi kwa kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari na kueleza kuwa ni imani yake kwamba timu ya TRA United itaendelea kufanya vizuri.







0 Comments