NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, amesema kuwa familia zina nafasi kubwa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kuhakikisha watoto wanapatiwa elimu ya kutosha kuhusu madhara ya matumizi ya dawa hizo tangu wakiwa katika umri mdogo.
Mapunda alitoa kauli hiyo leo Julai 23, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa tamasha la "Kataa Dawa za Kulevya, Timiza Malengo Yako", lililoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa lengo la kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya dawa za kulevya.
Amesema mafanikio ya vita dhidi ya dawa za kulevya hayatategemea tu kukamata wasafirishaji na wafanyabiashara haramu, bali pia kupunguza idadi ya watumiaji kwa kujenga uelewa kwa jamii, hususan watoto na vijana.
"Vita dhidi ya dawa za kulevya inahitaji juhudi za pamoja katika kukata njia za usambazaji, kuzuia biashara haramu na muhimu zaidi kupunguza idadi ya watumiaji. Pasipo kuwa na mahitaji, biashara hiyo itakosa soko," amesema Mapunda.
Ameongeza kuwa matumizi ya dawa za kulevya huanza taratibu kwa majaribio, lakini baadaye husababisha utegemezi unaoweza kuharibu afya, elimu, ajira na maisha ya mtumiaji.
"Hacheni kufuata mkumbo wa kujaribu kila jambo kwa kisingizio cha fasheni. Matumizi ya dawa za kulevya huanza kwa majaribio, lakini baadaye hugeuka utegemezi unaoharibu afya na maisha," amesisitiza.
Mapunda amewataka wazazi, walezi, walimu na jamii kwa ujumla kushirikiana katika kuwalea watoto kwenye maadili mema na kuwapatia elimu ya mara kwa mara kuhusu athari za dawa za kulevya ili kulinda kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Divisheni ya Dawa na Tina, Dk. Cassian Nyandindi akizungumza kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) amesema bado inahitajika elimu sahihi kwa umma kuhusu kukataa kuonja au kujaribu matumizi ya dawa za kulevya nchini.
Amesema jitihada za kutosha zinahitajika kuanzia ngazi ya kaya kwa vijana kuacha matumizi ya dawa za kulevya ili kuimarisha taifa letu.



0 Comments