Ticker

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA CCM YARIDHISHWA NA UTEKELEZWAJI WA UJENZI WA MADARAJA TABORA

Tabora

Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa madaraja inayosimamiwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) baada ya kukagua miradi hiyo katika Wilaya ya Igunga na Manispaa ya Tabora.

Ukaguzi huo umefanyika wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Mkoa ya kutathmini utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha miezi sita.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Ndugu Said Nkumba, amesema kuwa kamati imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa madaraja hayo na kuwataka wasimamizi wa miradi katika ngazi za wilaya na mkoa kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na miundombinu hiyo.

Aidha, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara nchini, akisema hatua hiyo inachochea ukuaji wa uchumi na kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa TARURA Mkoa wa Tabora, Mhandisi Baraka Mkuya amesema kuwa kukamilika kwa madaraja hayo kutarahisisha usafiri na usafirishaji wa watu pamoja na bidhaa, hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi na kupunguza vifo vinavyotokana na wananchi kuvuka mito wakati wa mvua.

Alieleza kuwa miradi iliyotembelewa ni Daraja la Igambilo–Igombe lenye urefu wa mita 27, lililogharimu shilingi milioni 590.4 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, na Daraja la Mawe la Nyandekwa–Mwabulele lenye urefu wa mita 25.5, lililogharimu shilingi milioni 203.8 kutoka Serikali Kuu kupitia mapato ya tozo za mafuta.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Tabora walieleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo, wakisema umeakisi utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha miezi sita. Waliwataka watendaji wa TARURA kuendelea kusimamia miradi hiyo kwab kuzingatia viwango vya ubora na kuwashirikisha wananchi katika kulinda na kutunza miundombinu hiyo mara baada ya kukamilika.

Post a Comment

0 Comments