NA EMMANUEL MBATILO, PWANI
WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amekabidhi gari la wagonjwa (ambulance) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, likiwa na lengo la kuimarisha huduma za dharura katika Kituo cha Afya Magindu na maeneo ya jirani.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Mchengerwa amesema ambulance hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita za kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa wakati, hususan wagonjwa wanaohitaji rufaa na matibabu ya haraka.
Amesema gari hilo litasaidia kuwasafirisha kwa usalama wagonjwa na majeruhi, wakiwemo wajawazito wenye dharura, watoto wachanga, waathirika wa ajali pamoja na wagonjwa wenye matatizo makubwa ya kupumua, magonjwa ya moyo, kiharusi na dharura nyingine.
“Katika dharura, kila dakika ina thamani. Dakika chache zinaweza kuwa tofauti kati ya uhai na kifo, au kati ya kupona na kupata ulemavu wa kudumu,” amesema Mchengerwa.
Amesema uwepo wa ambulance hiyo utasaidia kupunguza ucheleweshaji wa rufaa, kuongeza usalama wa wagonjwa wanapokuwa safarini na kuunganisha Kituo cha Afya Magindu na hospitali zenye huduma za juu zaidi.
Aidha ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kuhakikisha ambulance hiyo inatumika kwa shughuli za huduma za afya pekee na si kwa safari binafsi, shughuli za kiutawala au matumizi mengine yasiyohusiana na afya.
Aidha, ameitaka Halmashauri kuweka utaratibu wa matengenezo kinga pamoja na kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya mafuta, matengenezo, matairi, betri, bima na mahitaji mengine muhimu ya gari hilo.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuwepo kwa usimamizi na uwajibikaji wa moja kwa moja, huku taarifa za safari, matumizi ya mafuta, kilometa, tarehe za matengenezo na hitilafu zikitunzwa na kujadiliwa mara kwa mara.
Wakati huohuo, amewataka wananchi kulinda na kutumia kwa usahihi mali hiyo ya umma, akisisitiza kuwa ambulance inapaswa kutumika kwa kuzingatia uhitaji wa kitabibu bila ubaguzi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kungene, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuimarisha huduma za afya mkoani humo, huku akiipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kwa kupokea gari hilo la wagonjwa litakalosaidia kuongeza ufanisi wa huduma za dharura.
Kungene amesema kupatikana kwa ambulance hiyo ni hatua muhimu katika kuhakikisha wagonjwa, hasa wanaohitaji huduma za dharura na rufaa, wanawahi kufikishwa katika vituo vyenye uwezo wa kutoa huduma zaidi.
Aidha, amesisitiza kuwa huduma za afya ni msingi wa ustawi wa jamii, hivyo viongozi na wananchi wanapaswa kushirikiana kulinda miundombinu na vifaa vinavyowekezwa na Serikali kwa manufaa ya wananchi.
Amesema Serikali ya Mkoa wa Pwani itaendelea kushirikiana na Halmashauri zote kuhakikisha maboresho yanayofanyika katika sekta ya afya yanafika kwa wananchi na yanazaa matokeo yanayokusudiwa.
0 Comments