Ticker

6/recent/ticker-posts

MZUMBE YATOA USHAURI WA UCHAGUZI WA KOZI KATIKA KAMBI YA UDAHILI MLIMANI CITY

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

CHUO Kikuu Mzumbe kimewahimiza wanafunzi na wazazi kutumia fursa ya kambi maalumu ya udahili inayoendelea katika viwanja vya Mlimani City ili kupata ushauri wa kitaaluma na kufanya maamuzi sahihi kuhusu uchaguzi wa kozi za masomo ya juu.

Akizungumza katika kambi hiyo leo Agosti 2, 2026, Mkuu wa Kitengo cha Udahili wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam, Aziza Juma, amesema huduma zinazotolewa zinajumuisha elimu kuhusu uchaguzi wa kozi, vigezo vya kujiunga na chuo, ushauri wa kitaaluma pamoja na udahili wa papo kwa papo kwa waombaji wanaokidhi sifa.

Amesema kambi hiyo inalenga kuwasaidia wanafunzi kuelewa kwa kina kozi zinazotolewa na chuo na kuhakikisha wanaomba programu zinazolingana na sifa walizonazo.

"Tunatoa ushauri kuhusu uchaguzi wa kozi kwa sababu baadhi ya wanafunzi huomba programu ambazo haziendani na masomo waliyosoma shule, diploma au cheti. Tunawasaidia kufanya uchaguzi sahihi kulingana na sifa zao," amesema Aziza.

Ameongeza kuwa kambi hiyo pia ni fursa ya kuhamasisha jamii kufahamu programu mbalimbali zinazotolewa na Chuo Kikuu Mzumbe, kwani bado kuna watu wengi hawana taarifa za kutosha kuhusu fursa za masomo zinazopatikana chuoni hapo.

Kuhusu programu za teknolojia, amesema Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea kuimarisha masomo yanayohusiana na sayansi na teknolojia ili kuwaandaa wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya dunia ya sasa.

"Teknolojia ndiyo mwelekeo wa dunia ya leo. Tunawahamasisha vijana kujiandaa kwa kuchagua kozi zitakazowawezesha kupata ujuzi wa kisasa, kuchangia maendeleo ya jamii na kushindana katika soko la ajira," amesema.

Aziza amesisitiza kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kitaendelea kutoa elimu na ushauri kwa waombaji ili kuhakikisha wanafanya uchaguzi sahihi wa taaluma unaoendana na ndoto na uwezo wao wa kitaaluma.

Kambi hiyo imeanza Julai 28 hadi Agosti 3, 2026 ambapo hadi sasa muitikio unaridhisha kwa wananchi ambao wamepata fursa ya kutembelea eneo hilo na kupatiwa huduma.

Baada ya hapo zoezi litaendelea katika kampasi za Morogoro, Mbeya na hapa Dar es Salaam hivyo wazazi walezi wasisite kutembelea kampasi au kuomba online. 

Post a Comment

0 Comments