Ticker

6/recent/ticker-posts

NAIBU SPIKA SILLO AIPONGEZA IAA KUZINGATIA TEKNOLOJIA, SOKO KUTOA KOZI ZAKE

 


Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Daniel Sillo amekipongeza  Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa kuchukua hatua ya kuanzisha programu mpya na kuboresha programu zake katika  kuandaa wahitimu kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira.

 Mhe. Sillo ameyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa programu  za Shahada ya Uhasibu na Teknolojia ya Habari (Bachelor Degree in Accountancy with IT) na Shahada ya Sayansi ya Kompyuta(Bachelor Degree in Computer Science) katika Kampasi ya Babati  iliyofanyika Waangw’aray Mjini Babati.

Mhe. Sillo amesema Uzinduzi wa programu hizi mbili una umuhimu mkubwa katika safari ya kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025–2050, ambayo inalenga Tanzania yenye maendeleo jumuishi, yenye uchumi shindani, matumizi makubwa ya maarifa, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.

‘Ili kufikia malengo ya Dira hii,tunahitaji kuwekeza katika rasilimali watu wenye maarifa na ujuzi unaoendana na mabadiliko ya dunia. Tunahitaji wataalam ambao hawawezi tu kutumia teknolojia zilizopo pekee, bali wanaoweza kubuni teknolojia mpya, kuboresha mifumo na kutumia maarifa yao kutatua changamoto za Taifa,” amesema Mhe. Sillo.

Mkuu wa Chuo IAA, Prof. Eliamani Sedoyeka amesema kupitia programu hizi tunatarajia kupata wataalam wenye uwezo wa kuunganisha taaluma ya fedha na teknolojia, wabunifu, watengenezaji wa mifumo na wataalam wenye uwezo wa kutumia teknolojia kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.

Akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara na Mkuu wa Wilaya ya Babati, Katibu Tawala wa Wilaya ya Babati, Bw. Tobias Abwaro amepongeza IAA kuzindua kozi hizo ambazo zitafundishwa kisasa kuendana na matakwa ya kidunia ya kiteknolojia kutokana na uwekezaji wa miundombinu uliofanywa na Serikali chuoni hapo.

Post a Comment

0 Comments