Na Oscar Assenga, Kilindi
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Crispian Chalamila amemuahidi Rais Samia Suluhu Hassan kuwa taasisi hiyo itaendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi katika kuhakikisha vita dhidi ya rushwa nchini vinafanikiwa.
Chalamila alisema hayo wakati akizindua jengo jipya la ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Kilindi, mkoani Tanga, akisema Serikali imeendelea kuiwezesha taasisi hiyo kwa rasilimali watu, fedha na vitendea kazi ili kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa.
Alisema uwekezaji huo ni ishara ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia katika kuhakikisha TAKUKURU inakuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
“Kwa niaba ya menejimenti ya TAKUKURU, nitoe shukrani za dhati kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha taasisi hii kwa rasilimali watu, vitendea kazi na fedha,” alisema.
Chalamila alisema uwezeshaji huo umewezesha taasisi kujenga ofisi katika mikoa na wilaya mbalimbali, jambo linalowapa watumishi mazingira bora ya kufanyia kazi na wananchi kupata huduma kwa mazingira rafiki.
Ofisi 93 kufikia 2027
Chalamila alisema TAKUKURU imeweka mkakati wa kutenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya ujenzi wa ofisi zake, huku akieleza kuwa taasisi hiyo ina ofisi 145 katika mikoa yote 26, wilaya 111 na vituo maalumu sita.
Alisema kati ya ofisi hizo, majengo 70 yanamilikiwa na TAKUKURU na yanapatikana katika mikoa 23, wilaya 46 na kituo maalumu kimoja.
“Majengo yanayoendelea kujengwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 na 2026/2027 ni 23, ambayo yanajumuisha ofisi tatu za mikoa na ofisi 20 za wilaya,” alisema.
Alisema kukamilika kwa miradi hiyo kutafanya hadi mwaka 2027 TAKUKURU kuwa na majengo 93 yanayomilikiwa na taasisi hiyo.
Hata hivyo, alisema bado kuna ofisi 52 ambazo hazijafikiwa na mpango huo wa ujenzi, zikiwa katika mikoa miwili, wilaya 45 na vituo maalumu vitano.
Kwa upande wa jengo la TAKUKURU Kilindi, Chalamila alisema limegharimu Sh450.7 milioni hadi kukamilika, ikiwa ni ongezeko la Sh3.1 milioni, sawa na asilimia 0.7 ya bajeti ya awali.
Alisema ongezeko hilo lilitokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi.
Pia aliwataka watumishi wa TAKUKURU katika wilaya ya Kilindi na maeneo mengine yenye majengo mapya kuyatunza pamoja na vitendea kazi walivyopewa ili yaweze kutumika kwa muda mrefu.
“Serikali imewawezesha kwa kiwango kikubwa. Hilo ni deni ambalo tunapaswa kulilipa kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi zaidi ili dhamira ya Serikali ya kuitokomeza rushwa nchini itimie,” alisema.
DC aomba jenereta
Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Hashim Mgandilwa, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuziwezesha taasisi zake kuwa na miundombinu bora inayorahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mgandilwa alisema ujenzi wa jengo hilo ni hatua muhimu kwa wilaya hiyo, ambayo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002 imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya upungufu wa miundombinu ya ofisi.
Hata hivyo, aliomba TAKUKURU kuangalia uwezekano wa kuiwezesha ofisi hiyo kupata jenereta kutokana na changamoto ya kukatika kwa umeme katika eneo hilo.
“Jengo ni zuri, lakini haitakuwa na maana kama mwananchi akija kupata huduma anaambiwa umeme umekatika. Tunaomba muone namna ya kupata jenereta ili huduma ziendelee muda wote,” alisema.
Alisema Serikali tayari imeweka mpango wa kuimarisha umeme katika eneo hilo na imetenga Sh98 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo kidogo cha kupoza umeme.
TAKUKURU Kilindi yapata ofisi baada ya miaka 20
Kwa upande wake, Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga, Ramadhan Ndwatah, alisema kabla ya kupata jengo hilo, taasisi hiyo ilifanya kazi katika majengo ya kupanga kwa takribani miaka 20.
Alisema kuanzia mwaka 2005 hadi 2010 walikuwa katika majengo ya kupanga Kata ya Songe, kabla ya kuhamia Kata ya Bokwa, Kijiji cha Legeza Mwendo, ambako walikaa hadi mwaka 2026.
Ndwatah alisema hali hiyo ilisababisha changamoto mbalimbali, ikiwamo majengo kutokidhi mahitaji ya kisasa ya ofisi, changamoto za mawasiliano na ulazima wa kufanya ukarabati mara kwa mara.
Alisema pia kuwepo kwa ofisi katika majengo ya makazi ya watu kulikuwa kunawafanya baadhi ya wananchi kukosa uhuru wa kufika kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa utulivu.
“Tunamshukuru Mkurugenzi Mkuu kwa uamuzi wa kutujengea jengo hili la kisasa. Litasaidia wananchi wa Kilindi kufika kwa uhuru na kupata huduma katika mazingira bora,” alisema.
Jengo hilo jipya linatarajiwa kuongeza ufanisi wa TAKUKURU Wilaya ya Kilindi katika kutekeleza majukumu yake, ikiwamo kupokea taarifa na malalamiko ya wananchi kuhusu vitendo vya rushwa.
0 Comments