Na Mwandishi Wetu - Tanga
Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) inaendelea kushiriki katika Maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika katika Viwanja vya Usagara jijini Tanga, ikitumia jukwaa hilo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya mionzi na fursa zinazotokana na teknolojia ya nyuklia katika kuchochea maendeleo ya Taifa.
Maonesho hayo, yanayoratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, yanawakutanisha taasisi za Serikali, taasisi za elimu na utafiti, wabunifu, wanafunzi, wataalamu pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu, sayansi na teknolojia.
Katika banda la TAEC, wananchi, wanafunzi na wadau mbalimbali wanaendelea kupata elimu kuhusu jukumu la Tume la kusimamia na kudhibiti matumizi salama ya mionzi nchini, pamoja na mchango wa teknolojia ya nyuklia katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, kilimo, mifugo, maji, viwanda, migodi, utafiti na nishati.
Ushiriki wa TAEC katika maonesho hayo pia unatoa fursa kwa wanafunzi na vijana kufahamu taaluma mbalimbali zinazohusiana na teknolojia ya nyuklia na umuhimu wa kujikita katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM) ili kujenga kizazi cha wataalamu kitakachosaidia Taifa kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Akifungua rasmi maonesho hayo Agosti 18, 2026, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alisisitiza umuhimu wa elimu, ujuzi, sayansi, teknolojia na ubunifu katika kujenga uchumi wa kisasa na kuongeza uwezo wa Taifa kutumia maarifa na teknolojia katika kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo.
Katika muktadha huo, ushiriki wa TAEC unaunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha sayansi na teknolojia zinatumika moja kwa moja katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Teknolojia ya nyuklia ina matumizi mapana yenye manufaa kwa wananchi, ikiwemo katika uchunguzi na tiba ya magonjwa, kuongeza tija katika kilimo na mifugo, usimamizi wa rasilimali za maji, shughuli za viwandani na migodini, utafiti wa kisayansi pamoja na sekta ya nishati.
Wananchi wanaotembelea banda la TAEC pia wanapata nafasi ya kuzungumza moja kwa moja na wataalamu, kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu usalama wa mionzi, udhibiti wa vyanzo vya mionzi na matumizi ya teknolojia ya nyuklia kwa madhumuni ya amani na maendeleo.
TAEC itaendelea kutoa elimu na kuhamasisha matumizi salama ya mionzi na teknolojia ya nyuklia kwa maendeleo endelevu ya Taifa.
“Mionzi kwa Matumizi Salama na Teknolojia ya Nyuklia kwa Maendeleo ya Taifa."








0 Comments