SAB Investments, kampuni ya Kitanzania inayojihusisha na biashara ya kilimo na mifugo yenye makao makuu Dar es Salaam, kwa kushirikiana na kampuni za Uholanzi, inaendelea kuleta mageuzi katika sekta ya ufugaji wa kuku kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa na ushirikiano wa kimkakati unaolenga kuongeza tija kwa wafugaji nchini.
Katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea, kampuni hiyo inaonesha ubunifu mbalimbali katika uzalishaji wa chakula bora cha mifugo na teknolojia za kisasa za uchambuzi wa ubora wa chakula cha mifugo. Aidha, imetangaza kuwa tarehe 16 hadi 17 Oktoba 2026 itaandaa maonesho maalumu ya sekta ya kuku yatakayowakutanisha wadau mbalimbali wa ufugaji.
Akizungumza katika mahojiano maalumu, Mkurugenzi Mtendaji wa SAB Investments (SAB Feeds), Saida Bwanaheri, alisema sekta ya chakula cha mifugo nchini inaendelea kukua kwa kasi kutokana na kuongezeka kwa ufugaji wa kibiashara, mahitaji ya bidhaa bora na uelewa wa wafugaji kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa mifugo.
Alisema ili kasi hiyo iendelee, kuna haja ya kuwekeza zaidi katika mafunzo, suluhisho za kidijitali na ushirikiano wa kimataifa unaowezesha uhamishaji wa teknolojia na maarifa.
Bwanaheri alisema SAB Investments imefanikiwa kuongeza ubora wa bidhaa zake kupitia matumizi ya teknolojia ya skana ya Near Infrared (NIR), inayowezesha uchambuzi wa haraka na sahihi wa ubora wa malighafi na chakula cha mifugo kabla ya kuanza uzalishaji.
Kwa mujibu wake, teknolojia hiyo imepunguza utegemezi wa vipimo vya muda mrefu vya maabara, kuongeza usahihi wa maamuzi ya ununuzi wa malighafi, kupunguza hasara na kuimarisha ubora wa bidhaa zinazowafikia wafugaji.
Aidha, alisema kampuni hiyo imenufaika kwa kiwango kikubwa na mafunzo yanayotolewa na kampuni ya AgroCares ya Uholanzi, ambayo yamewaongezea wataalamu wao uwezo wa kutumia teknolojia hiyo, kufanya uchambuzi wa takwimu na kuimarisha mifumo ya uhakiki wa ubora wa chakula cha mifugo.
"Maarifa tuliyoyapata yametuwezesha kuboresha uundaji wa mchanganyiko wa chakula cha mifugo, kupunguza hatari za ubora na kufanya maamuzi yanayotegemea ushahidi, jambo ambalo limeongeza uzalishaji na faida," alisema.
Aliongeza kuwa kabla ya ushirikiano huo, changamoto kubwa ilikuwa kuhakikisha ubora wa malighafi kutoka kwa wasambazaji mbalimbali unabaki katika kiwango kinachofanana kutokana na tofauti za virutubisho.
Hata hivyo, kupitia teknolojia ya AgroCares, sasa uchambuzi wa ubora unafanyika papo hapo eneo la uzalishaji kabla ya malighafi kuingia kiwandani, hatua iliyoongeza ufanisi wa uzalishaji na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ubora.
Kwa upande wake, Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa AgroCares Afrika, Bw. Mukami Gitau, alisema kampuni hiyo imechagua kufanya kazi Tanzania kupitia SAB Investments kutokana na uzoefu wake mkubwa katika sekta ya mifugo na chakula cha mifugo.
Alisema AgroCares inaleta teknolojia ya kimataifa ya skana za uchambuzi wa chakula cha mifugo na ramani za udongo, huku SAB Investments ikisimamia utekelezaji wa teknolojia hiyo na kuwafikishia wafugaji suluhisho zinazotegemea takwimu.
Gitau alisema ushirikiano huo pia umechangia kuongezeka kwa ajira katika huduma za kiufundi, mauzo, mafunzo, huduma kwa wateja na usambazaji wa teknolojia za kisasa nchini.
Alieleza kuwa usimamizi bora wa ubora wa chakula cha mifugo unaongeza fursa za kiuchumi kwa wafugaji, wazalishaji wa chakula cha mifugo, wasafirishaji na wadau wengine wa mnyororo wa thamani wa mifugo.
Kwa mujibu wa viongozi hao, ushirikiano kati ya kampuni za ndani na washirika wa kimataifa umeonyesha kuwa uhamishaji wa teknolojia, ujenzi wa uwezo na ubunifu vina mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza kipato cha wafugaji nchini.
Kutokana na mafanikio hayo, SAB Investments imewataka watunga sera, taasisi za utafiti, washirika wa maendeleo na sekta binafsi kuendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa, mafunzo na ubunifu ili kuharakisha mageuzi ya sekta ya mifugo na kuifanya kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa Tanzania.


0 Comments