Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MBARAWA: MV LIEMBA IMEFIKA ASILIMIA 97, SAFARI KUANZA RASMI SEPTEMBA 1

     

Meli kongwe ya Mv Liemba iliyosimama kazi kwa zaidi ya miaka nane, imeanza rasmi majaribio ya kiufundi baada ya serikali kutumia shilingi bilioni 34 kufanya ukarabati na uwekezaji katika meli hiyo, inayotarajiwa kuanza safari zake September Mosi mwaka huu ikihudumia nchi jirani za Burundi, Zambia na Congo DRC.

Akizungumza baada ya kufanya majaribio ya meli hiyo Waziri wa Uchukuzi Makame Mbarawa, alisema majaribio yatafanyika kwa awamu mbili jana ikiwa ni awamu ya kwanza, kabla ya majaribio ya awamu ya mwisho yatakayofanyika kati ya tarehe 19-21 Agosti mwaka huu lengo ikiwa kupima mifumo muhimu kabla ya kuanza kwake.

‘Meli ya Mv Liemba itatumika miaka 50, ikifanyiwa matengenezo ya mara kwa mara itadumu zaidi ya miaka 80, leo tumeangalia ubora wa vifaa vyote na namna itakavyoweza kumudu kipindi cha dharura”, alisema Mbarawa.

Alisema meli hiyo imefanyiwa majaribio kwa viwango vya kimataifa, na baada ya hapo atakuja Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) ili kujiridhisha juu ya ubora kabla ya kutoa kibali cha kuanza kutumika.

“Katika jambo lililokuwa linatusumbua bungeni lilikuwa ni suala la meli ya Mv Liemba, sasa imekamilika, inakwenda kuondoa kero ya usafiri kwa wananchi wa mikoa ya pembezo mwa ziwa Tanganyika ikiwemo, Rukwa, Kigoma na Katavi, tunawaomba wananchi waitunze ili iweze kudumu kwa muda mrefu”, aliongeza Mbarawa.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) Erick Hamis, alisema meli hiyo imekuwa Liemba mpya kwakuwa wamerudisha asili ya zamani ya mbao ili kuweka asili yake sambamba na vifaa vingine kuwa vipya kama jenereta.

“Tunaishukuru serikali kwa kutulipa vizuri, tumemaliza mradi ndani ya muda kama tulivyoahidi, tunamshukuru mkandarasi kwa kufanya kazi yake vizuri, hii meli imekuwa kama mpya”, alisema Hamis.

Naye Rayton Kwembe, mkurugenzi wa Dar-es Salaam Merchant Group (DMG) mkandarasi mzawa aliyesimamia maboresho na ukaratbati wa MV Liemba, alisema kazi iliyofanyika ilihusisha kubadilisha mitambo yote ya uendeshaji, ikiwemo injini na jenereta, pamoja na sehemu za abiria, viti na vitanda, ambavyo vyote vimewekwa vipya.

“Tumefanya yote haya bila kuathiri historia ya meli hii, tumeacha jumba lake kama lilivyokuwa, kwa chini kulikuwa na mbao, tumerudisha kama ilivyokuwa kwa kuweka mbao mpya, ni meli ambayo, kwa umbo lake na historia yake imebaki vilevile ila kila kitu kimekuwa kipya”, alisema Kwembe.

Kwa kipindi chote ambacho meli ya MV Liemba ilikuwa chini ya matengenzo wakazi wanaozunguka ziwa Tanganyika walisema walikabiliwa na changamoto mbalimbali za usafiri na usafirishaji wa mzigo.

Musa Tulikubili alisema meli hiyo itawarahisihia wananchi wa mkoa wa Kigoma kusafirisha mazao kutoka vijiji vilivyopo mwambao mwa ziwa Tanganyika wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi na kilimo.

Meli ya Mv Liemba yenye uwezo wa kubeba abiria takribani 600 na mizigo yenye tani 200, sasa imefikia aslimia 97 za ukarabati  uliodumu kwa takribani miaka miwili toka 2024-2026.

Katika Ziara ya Waziri Mbarawa, amekagua pia upanuzi wa bandari ya Kigoma eneo la kuegesha meli za abiria, na chelezo la kujengea Meli katika ziwa Tanganyika ambapo alisema, serikali imedhamilia kufungua mkoa wa Kigoma kuwa kitovu cha biashara, ili kunufaika na uwepo wan chi jirani.

Post a Comment

0 Comments