
Na Mwandishi wa OTR - Arusha.
Serikali imesema Mkutano wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (C-CEOs Forum) 2026, unaotarajiwa kuwakutanisha viongozi kutoka Mashirika zaidi ya 300 ya Umma, pamoja na wawakilishi wa Sekta Binafsi na washiriki wengine zaidi ya 700 kuanzia Septemba 28 hadi 30, 2026, utakuwa jukwaa muhimu la kuimarisha utendaji, tija na mchango wa Mashirika hayo katika utekelezaji wa Dira 2050.
Forum hiyo, inayoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), ni ya nne kufanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023 na inalenga kuwakutanisha Wenyeviti wa Bodi, Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma na wadau mbalimbali kujadili namna ya kuongeza ufanisi wa taasisi hizo na kuhakikisha mipango na shughuli zao zinaendana na vipaumbele vya kitaifa vilivyoainishwa katika Dira 2050.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Ijumaa, Septemba 25, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, alisema kuwakutanisha viongozi wa Mashirika ya Umma katika jukwaa moja kunatoa fursa ya kujenga uelewa wa pamoja, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano kwa lengo la kuongeza tija na mchango wa Mashirika hayo katika maendeleo ya Taifa.
Amesema ni muhimu Mashirika ya Umma kuhakikisha mipango na shughuli zao zinaendana na malengo ya Dira 2050, ili rasilimali na uwekezaji unaosimamiwa na Serikali uweze kuzalisha matokeo yenye thamani zaidi kwa uchumi na wananchi.
“Tunataka mkutano huu uwe na manufaa yanayoonekana pia nje ya ukumbi wa mikutano, kwa kuwafungulia fursa wafanyabiashara, watoa huduma na wananchi wa Arusha,” alisema.
Mhe. Makalla amesema Arusha ina uzoefu wa kuhudumia mikutano mikubwa ya kitaifa na kimataifa na kwamba Mkoa uko tayari kuwapokea washiriki wa C-CEOs Forum 2026, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mazingira ya usalama, utulivu na ukarimu kwa wageni.
“Watakaohudumia wageni wawe wakarimu ili warudi tena,” amesema, akieleza kuwa ujio wa washiriki zaidi ya 700 utatoa fursa kwa sekta mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo hoteli, migahawa, usafiri, utalii, biashara na huduma nyingine.

Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alisema utekelezaji wa Dira 2050 unahitaji mabadiliko katika namna Mashirika ya Umma yanavyotazama utendaji wao, kutoka kwenye kuendesha taasisi na shughuli zake kwenda kwenye kuzalisha matokeo yanayopimika na yenye thamani kwa Taifa.
Kwa mtazamo wake, ufanisi wa juu unapaswa kuonekana katika uwezo wa Mashirika kutumia rasilimali na uwekezaji waliokabidhiwa kwa tija, kujenga ushindani, kuimarisha uimara wa kifedha na kutoa huduma zenye ubora, huku yakichangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi.
“Tunataka Mashirika ya Umma yenye ufanisi wa juu, shindani na imara katika kutekeleza Dira 2050,” alisema Mchechu.
Bw. Mchechu alisema thamani ya uwekezaji wa Serikali katika Mashirika na kampuni zake imeongezeka kutoka Sh67.95 trilioni mwaka 2020/21 hadi Sh92.28 trilioni mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 35.8, hali inayoongeza umuhimu wa kuhakikisha uwekezaji huo unazalisha matokeo makubwa zaidi.
Alisema matokeo hayo hayawezi kupimwa kwa gawio pekee, bali yanapaswa kuangaliwa kwa upana kupitia tija, ubora wa huduma, ufanisi wa matumizi ya rasilimali, uimara wa kifedha, ubunifu, matumizi ya teknolojia, uwezo wa kushindana na athari ya taasisi katika uchumi.
Kwa mtazamo huo, alisema Mashirika ya Umma yanapaswa kujenga uwezo wa kubadilika kulingana na mazingira ya uchumi, teknolojia na mahitaji ya wananchi, huku uongozi na bodi zikibeba jukumu muhimu la kuweka mwelekeo wa utendaji na uwajibikaji.
“C-CEOs Forum inalenga kuangalia kwa upana zaidi jinsi ya kubadilisha rasilimali na uwekezaji kuwa utendaji na matokeo yenye thamani zaidi,” alisema.
Bw. Mchechu alisema ongezeko la mapato yasiyo ya kodi linalotokana na Mashirika na taasisi zinazochangia kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, linaonesha pia umuhimu wa kuendelea kuboresha utendaji wa taasisi hizo.
Mapato hayo yameongezeka kutoka Sh637.7 bilioni mwaka 2020/21 hadi Sh1.327 trilioni mwaka 2025/26, sawa na ongezeko la asilimia 108.3.
Alisema kwa hiyo, mjadala kuhusu Mashirika ya Umma haupaswi kuishia kwenye suala la kiasi cha fedha kinachowasilishwa Serikalini, bali unapaswa kuangalia thamani pana inayozalishwa na uwekezaji wa umma, ikiwemo huduma, ajira, uzalishaji, ubunifu, ushindani na mchango katika uchumi.
Katika mtazamo wake, maeneo hayo yanahitaji uongozi wenye mwelekeo wa kimkakati, utawala bora, matumizi makubwa zaidi ya teknolojia za kidijitali na akili bandia, mifumo endelevu ya upatikanaji wa fedha, pamoja na ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.
Alisema pia Mashirika yanahitaji kuwekeza katika rasilimali watu na ujuzi wa baadaye ili yaweze kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia, kiuchumi na kimazingira, sambamba na kuzingatia masuala ya mazingira, jamii na utawala bora.

0 Comments