Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

C-SDTP YAZIDI KUIMARISHA UNYWAJI WA MAZIWA SHULENI KWA LISHE NA AFYA BORA

Mtaalamu wa Lishe kutoka Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP), Dkt. Mackrina Nombo, amesema mpango wa kuhamasisha unywaji wa maziwa shuleni unalenga kuongeza uelewa wa wanafunzi kuhusu umuhimu wa maziwa katika lishe bora, afya na ukuaji wao.

Akizungumza na vyombo vya habari, Dkt. Nombo amesema mwaka huu mpango huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa katika shule 18 za Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo shule 13 zipo Tanzania Bara.

Amesema utekelezaji wake utahusisha ushirikiano wa Serikali na wadau mbalimbali katika kuhakikisha wanafunzi wanapata maziwa kwa urahisi na kwa usalama wakiwa shuleni.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Bi. Deorinidei Mng’ong’o ambaye ni Kaimu Meneja Ufundi Maziwa, amesema Serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuhakikisha watoto wanapata lishe bora wakiwa shuleni, akieleza kuwa chakula bora, ikiwemo maziwa, ni sehemu muhimu katika kujenga afya ya mwili na akili na kuwawezesha watoto kushiriki vizuri katika masomo.

Bi. Mng’ong’o amesema watoto hutumia sehemu kubwa ya muda wao shuleni, hivyo kuna umuhimu wa kuweka mazingira yatakayowawezesha kupata mlo kamili na lishe yenye virutubisho muhimu kwa ajili ya ukuaji na maendeleo yao.

Amesema kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo Bodi ya Maziwa Tanzania, imeendelea kuweka mikakati ya kuhamasisha utekelezaji wa Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni kwa njia shirikishi, ambapo wazazi kupitia kamati za shule wanatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa mpango huo.

Katika hatua hiyo, Serikali na wadau wanatarajiwa kuunganisha shule na wasindikaji wa maziwa waliopo katika maeneo husika, sambamba na kuweka mazingira na miundombinu itakayorahisisha upatikanaji wa maziwa kwa wanafunzi shuleni.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotajwa na wadau wa Tasnia ya Maziwa, kiwango cha matumizi ya maziwa nchini bado kiko chini ya lengo linalotajwa kimataifa la wastani wa lita 200 kwa mtu kwa mwaka, huku matumizi nchini yakitajwa kuwa takribani lita 71 kwa mtu kwa mwaka.

Hivyo, utekelezaji wa Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni unatarajiwa kuwa miongoni mwa hatua za kuongeza uelewa na kuchochea matumizi ya maziwa nchini.

Post a Comment

0 Comments