MAMLAKA ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imetangaza mpango wa kukamata na kuchunguza maiti zitakazobainika kutumika katika usafirishaji wa dawa za kulevya nchini.
Kamishna Mkuu wa DCEA, Kamishna Aretas Lyimo, amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya oparesheni ya miezi mitatu iliyofanyika katika mikoa 14 nchini kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu.
Amesema katika oparesheni hiyo, DCEA imebaini baadhi ya maiti kusafirishwa kuelekea Kanda ya Kaskazini zikitumika kuficha na kusafirisha dawa za kulevya, hususan mirungi na bangi.
“Tutazikamata maiti zote zitakazohusika na usafirishaji wa dawa hizo, pamoja na magari na watu watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo,” amesema.
Katika oparesheni hiyo, DCEA imekamata jumla ya kilogramu 18,078.41 za dawa za kulevya katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Morogoro, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Dodoma, Mbeya, Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Lyimo amesema Morogoro na Tabora zimeendelea kubainika kuwa miongoni mwa maeneo yanayolima bangi kwa wingi, huku mamlaka ikiendelea kuchukua hatua kudhibiti uzalishaji na usafirishaji wa zao hilo.
Aidha, amesema pikipiki zimebainika kutumika zaidi katika kusafirisha bangi, ambapo DCEA imekamata pikipiki 40, bajaji moja na magari nane yaliyohusishwa na usafirishaji wa dawa za kulevya.
Amesema miongoni mwa magari hayo ni Toyota Harrier, Toyota Land Cruiser, Toyota IST, Toyota Noah, Toyota Alphard na Toyota Discovery, pamoja na basi la Kampuni ya Ratco lenye namba T.443 lililokamatwa likisafirisha bunda 238 zenye uzito wa kilogramu 125.33 kutoka Tanga kwenda Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, Lyimo amesema DCEA imekamata raia sita wa kigeni, wakiwemo raia wawili wa Afrika Kusini waliokuwa na gramu 65.8 za bangi, raia mmoja wa Kenya akiwa na gramu 3.89 za mirungi, raia mmoja wa Nigeria akiwa na gramu 4.6 za bangi na raia mmoja wa Uturuki aliyekuwa na gramu 1.87 za skanka.
0 Comments