Dodoma | Septemba 23, 2026
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Hassan Saidy, amesema Serikali imedhamiria kukamilisha miradi ya kusambaza umeme katika vitongoji vyote ifikapo mwaka 2030, hatua ambayo itachochea shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi.
Mha. Saidy ameyasema hayo leo jijini Dodoma, wakati akizungumza katika Kikao Kazi cha Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kilicholenga kujadili utekelezaji wa majukumu, maendeleo ya miradi pamoja na kuimarisha usimamizi ili kuhakikisha malengo ya Wakala yanafikiwa kwa wakati.
Akisisitiza umuhimu wa wajibu walio nao watumishi katika kutekeleza dhamira ya Serikali ya kufikisha nishati vijijini, Mha. Saidy amesema, “Tumebeba matumaini ya wananchi,” akiwataka watumishi kutambua kuwa mafanikio ya miradi yanagusa moja kwa moja maisha na shughuli za maendeleo za wananchi.
Aidha, Mha. Saidy amewataka wasimamizi wa miradi kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji na uadilifu, sambamba na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi katika maeneo yao na kuhakikisha changamoto zinazoweza kuchelewesha miradi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Amesisitiza kuwa ushirikiano, ufuatiliaji madhubuti na uwajibikaji wa kila mtumishi ni muhimu katika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa na kukamilika kwa wakati, ili wananchi waweze kunufaika na huduma ya umeme na kuitumia katika shughuli za uzalishaji na maendeleo.
Kupitia utekelezaji wa miradi hiyo, REA inaendelea kuimarisha juhudi za Serikali za kupanua wigo wa upatikanaji wa nishati vijijini, huku ikihimiza matumizi yenye tija ya umeme ili huduma hiyo iwe chachu ya kuinua uchumi wa wananchi na kuharakisha maendeleo katika maeneo ya vijijini.


0 Comments