Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

TAEC YAONGEZA NGUVU USALAMA WA MIONZI MIPAKANI, WATAALAMU WAPEWA MAFUNZO MAALUM


TUME ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imeendelea kuimarisha usalama wa mionzi na nyuklia katika mipaka ya nchi kwa kuwajengea uwezo wataalamu wake kuhusu uendeshaji, matengenezo na utunzaji wa vifaa vinavyotumika kugundua mionzi katika maeneo mbalimbali ya kuingia na kutoka nchini.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha vifaa vilivyowekwa katika maeneo ya kimkakati mipakani vinafanya kazi kwa ufanisi na vinaendelea kuwa katika hali nzuri wakati wote, ili kusaidia kubaini uwepo wa vifaa vya mionzi au nyuklia vinavyoweza kuingizwa au kusafirishwa nchini bila kufuata taratibu zinazotakiwa.

Akizungumza jijini Mwanza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Teknolojia na Huduma za Ufundi wa TAEC, Dkt. Remigius Kawala, amesema Tume imeendelea kuwekeza katika vifaa na miundombinu ya kisasa ili kuongeza uwezo wake wa kutoa huduma za kitaalamu kwa usahihi na kwa viwango vinavyokubalika.

Amesema katika mwaka huu wa fedha, TAEC imenunua vifaa mbalimbali vya maabara vyenye thamani ya takribani Sh bilioni 3, ikiwa ni sehemu ya uwekezaji unaolenga kuimarisha uwezo wa Tume katika kufanya vipimo, uchunguzi na tafiti mbalimbali zinazohusiana na matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia.

Kwa mujibu wa Dkt. Kawala, wataalamu wamekutana kwa siku mbili katika Kanda ya Ziwa kujitathmini kuhusu namna huduma za maabara zinavyotolewa, hali na ubora wa vifaa vinavyotumika pamoja na kuweka mikakati ya kuhakikisha vipimo vinavyofanyika vinakuwa sahihi na vya kuaminika.

“Tumekutana wataalamu Kanda ya Ziwa kwa lengo la kuweka mikakati ya utoaji wa huduma za maabara kwa usahihi bila kuwa na mashaka. Hivi ni vipimo ambavyo vinapaswa kuendana na viwango vinavyotambulika duniani,” amesema Dkt. Kawala.

Ameeleza kuwa TAEC ina takribani maabara tano katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Zanzibar, huku pia ikitoa huduma katika maeneo mbalimbali ya mipakani. Kutokana na ukubwa wa majukumu hayo, uwekezaji katika vifaa vya kisasa na kuwajengea uwezo wataalamu ni muhimu katika kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa na ubora unaotakiwa.

Katika mafunzo hayo, wataalamu wamejengewa uwezo wa kuendesha kwa usahihi vifaa vya kugundua mionzi vilivyowekwa mipakani, kufanya ukaguzi na matengenezo ya kawaida pamoja na kuvihifadhi na kuvitunza ili viweze kufanya kazi kwa ufanisi kwa muda mrefu.

Mafunzo hayo pia yameweka mkazo katika namna ya kutambua na kuchukua hatua pale vifaa vinapotoa tahadhari ya uwepo wa mionzi, sambamba na kuzingatia taratibu za kujikinga na mionzi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Vifaa hivyo vina umuhimu mkubwa katika mfumo wa usalama wa nchi kwa kuwa vinasaidia kugundua na kuzuia usafirishaji usioidhinishwa wa vifaa vya mionzi na nyuklia kupitia mipaka na maeneo mengine ya kimkakati ya kuingia na kutoka nchini.

Dkt. Kawala amesema uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali unalenga kuhakikisha TAEC inakuwa na uwezo wa kufanya vipimo, uchunguzi na tafiti mbalimbali kwa kutumia vifaa vya kisasa, huku matumizi ya teknolojia ya nyuklia yakifanyika kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa vya usalama.

Ameongeza kuwa teknolojia ya nyuklia haipaswi kuonekana kama eneo linalohusu kundi fulani la wataalamu pekee, kwa kuwa matumizi yake yana mchango katika maisha ya wananchi kupitia sekta mbalimbali zikiwemo afya, kilimo, viwanda, mazingira na utafiti.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TAEC, Bw. Peter Ngamilo, amesema pamoja na uwekezaji unaofanywa katika vifaa na kuwajengea uwezo wataalamu, Tume itaendelea kutoa elimu kwa umma ili wananchi waelewe umuhimu wa matumizi salama ya mionzi na teknolojia ya nyuklia katika maendeleo ya Taifa.

“Ni muhimu wananchi waelewe kuwa teknolojia ya nyuklia ina matumizi mengi yenye manufaa katika maisha yetu. Jukumu letu ni kuhakikisha matumizi hayo yanafanyika kwa usalama, lakini pia wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu kazi zinazofanywa na TAEC katika kuwalinda wao na mazingira dhidi ya madhara yanayoweza kutokana na matumizi yasiyo salama ya mionzi,” amesema Ngamilo.

Amesema uwepo wa vifaa vya kugundua mionzi katika maeneo ya mipakani ni sehemu muhimu ya mfumo wa ulinzi na usalama, kwa kuwa unasaidia kuhakikisha vifaa vya mionzi vinavyoingia au kutoka nchini vinatambuliwa na kushughulikiwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Aidha, Serikali imeendelea kuweka mazingira yanayowezesha taasisi za umma na sekta binafsi kushirikiana katika matumizi ya teknolojia ya nyuklia kwa madhumuni ya amani na maendeleo, ili manufaa ya teknolojia hiyo yaweze kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kawala amesema TAEC ipo katika hatua za mwisho za kupata ithibati zinazohitajika kwa ajili ya maabara yake kubwa na ya kisasa iliyopo jijini Arusha. Kukamilika kwa hatua hiyo kutaongeza uwezo wa maabara hiyo kutoa huduma za vipimo na uchunguzi kwa kuzingatia viwango vinavyotambulika.

Maabara hiyo inatarajiwa kuongeza uwezo wa Tanzania kufanya vipimo na tafiti za kitaalamu nchini na hivyo kuimarisha upatikanaji wa huduma zinazohusiana na teknolojia ya nyuklia pamoja na kupunguza utegemezi wa baadhi ya huduma kutoka nje ya nchi.

TAEC imeendelea kuimarisha uwezo wa Taifa katika usalama wa mionzi na nyuklia kupitia uwekezaji katika vifaa na miundombinu, mafunzo kwa wataalamu, usimamizi wa matumizi salama ya mionzi pamoja na ushirikiano na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Hatua hizo zinalenga kuhakikisha teknolojia ya nyuklia na mionzi inaendelea kutumika kwa usalama na kwa madhumuni ya amani, huku afya ya wananchi, wafanyakazi na mazingira ikilindwa.

Post a Comment

0 Comments