Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

TAFITI NA GUNDUZI ZA WANASAYANSI CHIPUKIZI ZINAUNGA MKONO LENGO LA KUANZISHA SHULE ZA AMALI - PROF. SHEMDOE

Na: OWM – TAMISEMI, Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema tuzo za tafiti na gunduzi katika maeneo ya ubunifu, sayansi, kilimo, nishati, mazingira na afya zinazotolewa kwa wanasayansi chipukizi na Shirikisho la Wanasayansi Chipukizi (Young Scientist Tanzania), zinaunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kujenga zaidi ya shule 103 za amali nchini.

Amesema shule hizo za amali zinalenga kuwapatia wanafunzi elimu inayowaunganisha moja kwa moja na ujuzi wa vitendo, ajira na fursa za kujiajiri.

Prof. Shemdoe ameyasema hayo Septemba 17, 2026, katika Ukumbi wa Maktaba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mara baada ya kutembelea na kujionea tafiti na gunduzi mbalimbali zilizofanywa na wanasayansi chipukizi kutoka shule za sekondari mbalimbali nchini, ambapo aliwatunuku tuzo wanafunzi walioibuka washindi.

“Nina imani tafiti na gunduzi nilizoziona hapa ndizo zinazopaswa kupewa kipaumbele katika utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, pamoja na mtaala ulioboreshwa. Wanasayansi hawa chipukizi wakimaliza shule watakuwa katika nafasi nzuri ya kutumia ujuzi wao kujiajiri,” amesema Prof. Shemdoe.

Amefafanua kuwa tuzo hizo pia zinaunga mkono utekelezaji wa Mpango wa Ufadhili wa Masomo wa Samia (Samia Scholarship), unaolenga kuwawezesha wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo ya sayansi, teknolojia, hisabati na ubunifu.

Prof. Shemdoe amesema ametembelea maonesho ya tafiti na gunduzi za wanasayansi hao chipukizi na kubainisha kuwa namna walivyojiandaa na kuwasilisha kazi zao ilikuwa ya kiwango cha juu kiasi kwamba mtu anaweza kudhani ni wanafunzi wa vyuo vikuu na si wanafunzi wa shule za sekondari.

Kutokana na hilo, amewapongeza waasisi wa tuzo hizo kupitia Shirikisho la Wanasayansi Chipukizi (Young Scientist Tanzania) kwa kuendelea kuwaibua na kuwajengea uwezo vijana katika tafiti, sayansi na ubunifu.

Akieleza sababu ya kushiriki katika tuzo hizo, Prof. Shemdoe amesema amefanya hivyo kwa kuwa Shirikisho la Wanasayansi Chipukizi linaratibu utoaji wa tuzo hizo kwa vijana ambao ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, ambazo ziko chini ya usimamizi wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, ambayo amepewa dhamana ya kuisimamia kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba.

Kwa upande wake, Mwanzilishi Mwenza wa Shirikisho la Wanasayansi Chipukizi (Young Scientist Tanzania), Dkt. Godbless Kamugisha, amesema tuzo hizo zimewakutanisha wanasayansi chipukizi kutoka shule za sekondari za mikoa mbalimbali ya Tanzania kwa ajili ya kuonesha kazi zao za tafiti na gunduzi zinazolenga kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili jamii katika maeneo ya kilimo, nishati, mazingira na afya.

Dkt. Kamugisha amesema jumla ya gunduzi 45 zimeoneshwa katika maonesho hayo, kati ya gunduzi 1,330 zilizowasilishwa na wanafunzi kwa ajili ya kushindania tuzo hizo.

Aidha, ameomba Serikali iendelee kutoa ushirikiano kwa Shirikisho hilo ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoshiriki katika mashindano hayo na kukuza ushindani miongoni mwa vijana katika tafiti, sayansi na ubunifu.

Post a Comment

0 Comments