Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

TANROADS YAAGIZA MAMENEJA 26 KUJIPANGA KUKABILI MVUA ZA EL NIÑO



Na Boniphace John, OKULY BLOG - DODOMA


Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umewaagiza Mameneja wa Mikoa yote 26 nchini kufanya ukaguzi wa miundombinu ya barabara, madaraja, makalavati na maeneo mengine hatarishi, ili kuchukua hatua za haraka kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.

Wito huo umetolewa jijini Dodoma Septemba 7,2026 na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa barabara ya Ntyuka–Mvumi–Kikombo pamoja na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo.

Mhandisi Besta amesema TANROADS inapaswa kuwa makini kwa kutambua mapema maeneo yanayoweza kuathiriwa na mvua na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kabla ya mvua kuanza.

Amesema ukaguzi huo ni muhimu kutokana na changamoto zilizowahi kujitokeza katika baadhi ya maeneo wakati wa mvua, akitoa mfano wa Daraja la Mutikila ambalo Desemba mwaka jana liliathiriwa na mvua na kusababisha usafiri wa magari na wananchi kukwama.

 “Natoa rai kwa mameneja wote wa mikoa 26 waende wakafanye ukaguzi na kuangalia ni namna gani wanaweza kupunguza athari zinazoweza kutokana na mvua za El Niño,” amesema Mhandisi Besta.

Amesema pamoja na Daraja la Mutikila, TANROADS inahakikisha kazi katika madaraja ya Mangungo na Kikombo, pamoja na madaraja mengine yanayotekelezwa katika mradi huo, zinakamilishwa kwa wakati ili yaweze kupitika wakati wa mvua.

Mhandisi Besta pia amemtaka mkandarasi wa mradi huo kuongeza kasi ya utekelezaji wa kazi ili kukamilisha sehemu iliyobaki na kuwawezesha wananchi kunufaika na barabara hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, mradi huo una urefu wa jumla ya kilomita 76 na unatekelezwa kwa awamu mbili.

Amesema awamu ya kwanza inayotekelezwa sasa inahusisha kilomita 25 na imefikia asilimia 67.9 ya utekelezaji.

Kati ya kilomita hizo, kilomita 8.6 ziko upande wa Ntyuka kuelekea Mvumi, huku upande wa Kikombo ukiwa na kilomita 14.4, ikiwemo kilomita tano zinazounganisha barabara hiyo na barabara inayoelekea Makao Makuu ya Jeshi.

Mhandisi Amani amesema mkandarasi wa mradi huo ni CHICO, ambaye tayari amekamilisha ujenzi wa sehemu kubwa ya barabara, ambapo kilomita 23.2 kati ya 25 zimefikia kiwango kinachohitajika.

Amesema kazi kubwa zilizobaki ni pamoja na kujaza tuta la barabara, kuunganisha maeneo ya madaraja na kukamilisha miundombinu ya kupitisha maji katika maeneo ya Mutikila, Mangungo na Kikombo, pamoja na daraja la reli ya MGR.

Amesema TANROADS tayari imeanza kuimarisha maeneo ya madaraja yaliyokuwa yakileta changamoto wakati wa mvua kwa kutumia kifusi, kuimarisha kingo za matuta na kufungua njia za mito, hatua inayolenga kuhakikisha watumiaji wa barabara wanaendelea kupita kwa usalama.

Kwa mujibu wa Mhandisi Amani, TANROADS inatarajia madaraja ya Mutikila, Mangungo na Kikombo kukamilika na kufikia hatua ya kupitika kabla ya kuanza kwa mvua, hatua ambayo itasaidia kupunguza usumbufu kwa wananchi na watumiaji wengine wa barabara.












Post a Comment

0 Comments