
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, amesema katika kipindi cha miezi michache iliyopita nchi hizi mbili zimepiga hatua katika sekta muhimu tano na kuweka matumaini ya ushirikiano zaidi katika sekta zingine.
Akizungumza leo asubuhi na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya Algeria kwenye ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Algiers, Balozi Matinyi alizitaja sekta hizo ambazo Ubalozi umefanikisha zipige hatua kuwa ni za viwanda vya dawa za tiba, nishati, elimu ya juu, biashara ya mazao ya kilimo na ufugaji wa nyuki.
Balozi Matinyi alisema juhudi za sasa za serikali za nchi hizi mbili zinafuatia maelekezo ya marais wa nchi hizi kwamba baada ya kuainisha maeneo ya ushirikiano baina ya Tanzania na Algeria sasa ni wakati wa kuyaweka katika vitendo kwa maendeleo ya wananchi wake.
“Nilipowasilisha hati zangu za utambulisho mnamo tarehe 10 Juni, 2026, Rais Abdelmadgid Tebboune alisisitiza kwamba sasa umefika wakati wa kuuweka ushirikiano wetu katika vitendo na wakati nikija Algeria Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliagiza kwamba kutokana na ushirikiano wetu wa kimkakati sasa ni wakati wa kupata manufaa kwa ajili ya wananchi wetu” alisema Balozi Matinyi.
Akielezea mafanikio hayo, Balozi Matinyi alisema katika sekta ya viwanda vya dawa za tiba Mamlaka ya Taifa ya Bidhaa za Dawa ya Algeria (ANPP) na kiwanda cha dawa cha Serikali ya Algeria cha Saidal Group, zitafanya ziara nchini mwezi Oktoba kwa mwaliko wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba ya Tanzania (TMDA) ili kujadili namna ya kushirikiana kitaalamu.
Balozi Matinyi alisema kwa kuzingatia kuwa katika ukaguzi wa dawa Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufikia kiwango cha juu (ML3) mwaka 2018 kwa mujibu wa tathmini ya kimataifa (GBT) ya Shirika la Afya la Dunia (WHO) huku Algeria ikiwa na theluthi moja ya viwanda 690 vya dawa Afrika, nchi hizi mbili zinaweza kufikia mafanikio makubwa.
“Kampuni ya dawa ya Hikma nayo ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha makubaliano ya ushirikiano katika biashara na uwekezaji na kampuni tanzu ya Bohari Kuu la Dawa (MSD) ya Medipharm ili kuhudumia nchi za ukanda wa mashariki, kati na kusini mwa Afrika,” alisema Balozi Matinyi na kuongeza: “Kampuni nyingine binafsi ya Frater Razes inakuja nchini mwezi Oktoba pia kujadiliana na Serikali namna ya kuanza ushirikiano katika biashara na uwekezaji,” alisema Balozi Matinyi.
Katika sekta ya nishati Balozi Matinyi alisema Kampuni ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO) ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), ilifanya ziara nchini Algeria mwezi Julai kujadiliana namna ya kushirikiana kiufundi na kutembelea maeneo ya kiufundi ya Shirika la Umeme na Gesi la Algeria (SONELGAZ) na kiwanda cha vifaa vya umeme cha GISB Electric.
Katika ushirikiano kwenye sekta ya elimu Balozi Matinyi alisema: “Algeria ilitoa nafasi 176 za masomo ya juu kwa wanafunzi wa Tanzania ambapo Serikali imeamua kuchagua wanafunzi wenye ufaulu wa juu 150 chini ya mpango wa Samia Scholarship Extended na wanakuja kwa ajili ya masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na tiba.”
Akizungumzia ushirikiano kwenye biashara ya mazao ya kilimo, Balozi Matinyi aliitaja kampuni ya Sarl Anacard’Or ya Algeria kwamba imenunua ghala la kuhifadhia korosho mkoani Mtwara kwa ajili ya kuzileta Algeria. Kampuni hiyo pia inakamilisha mipango ya kuanza ubanguaji korosho nchini Tanzania.
Aidha, Balozi Matinyi alisema kampuni nyingine ya Algeria ya kutengeneza mashine za kusindika mazao ya kilimo na dawa pamoja na kufungasha ya CAM Sarl imekubali kutoa ushirikiano kwa Tanzania wa kupata mashine hizo ili kuongezea thamani mazao ya kilimo kabla ya kuuzwa kwenye soko la dunia.
Balozi Matinyi alitaarifu zaidi kuwa Tanzania na Algeria zinatarajia kuanza ushirikiano katika sekta ya ufugaji wa nyuki na mazao yake kufuatia ziara ya maafisa na wataalamu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) pamoja na wadau wa sekta binafsi mwezi Septemba 2026 ambapo walikubaliana na wenzao wa Algeria kuanza ushirikiano.
Balozi Matinyi alimaliza taarifa yake kwa waandishi wa Algeria kwa kuwakaribisha wananchi wa Algeria kuja nchini kujionea fahari ya hifadhi za bonde la Ngorongoro na Serengeti, mlima Kilimanjaro na vilevile kuja kufurahia fukwe maridhawa za Zanzibar.
Algiers, Septemba 30, 2026.
0 Comments