VIJANA nchini wametakiwa kupewa mafunzo ya uongozi tangu wakiwa katika umri mdogo ili kuwaandaa kuwa viongozi wenye maadili, uwajibikaji na uwezo wa kuongoza katika nyanja mbalimbali, hatua inayolenga kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Wito huo umetolewa wakati Shirika la African Leadership Initiatives for Impact (ALII), kwa kushirikiana na HakiElimu na kwa uwezeshaji wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania, Norwegian Church Aid na UTT AMIS, likizindua awamu ya pili ya Programu ya Tanzania NextGen Leaders Fellowship (TNLF Cohort 2).
Programu hiyo inalenga kuwaandaa vijana kuwa viongozi wenye maono, maadili na uwezo wa kuchangia katika maendeleo ya taifa.
Uzinduzi wa programu hiyo ulifanyika leo katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ukihudhuriwa na vijana 100 waliochaguliwa kushiriki katika kundi hilo, pamoja na viongozi, wataalamu, wadau wa maendeleo na wawakilishi wa taasisi mbalimbali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Dkt. Redmond Mapana, amesema uwekezaji katika kuwajengea vijana uwezo wa uongozi tangu mapema ni muhimu katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na kizazi cha viongozi wenye uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na kukabiliana na changamoto za maendeleo.
Amesema programu hiyo inawapa vijana fursa ya kujifunza misingi ya uongozi, uzalendo, maadili na uwajibikaji, hivyo kuwataka kutumia maarifa watakayoyapata katika mafunzo hayo kujijengea uwezo na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Dkt. Mapana amesema ushiriki wa vijana katika masuala ya maendeleo ni muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea utekelezaji wa malengo yaliyowekwa kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Mary Ndaro, amesema programu hiyo imewakutanisha zaidi ya vijana 100 kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwapatia maarifa katika nyanja mbalimbali, hususan uongozi.
Amesema mafunzo hayo yanatoa fursa kwa vijana kubadilishana uzoefu, kujifunza kutoka kwa wataalamu na kujenga uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika jamii.
Aidha amesema uwekezaji katika kuwaandaa vijana kuwa viongozi bora ni hatua muhimu katika kujenga kizazi chenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii na taifa.
Kwa mujibu wa waandaaji, TNLF inalenga kuwajengea vijana ujuzi, mtazamo na misingi ya uongozi itakayowawezesha kuwa sehemu ya mabadiliko chanya katika jamii, huku wakitumia uwezo wao katika kuchangia maendeleo ya Tanzania.
0 Comments