Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

WADAU WAHIMIZWA MATUMIZI SAHIHI YA AI KATIKA SEKTA YA UTALII



Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Nkoba Mabula amewahimiza wadau wote wa utalii kuhakikisha wanaendana na mabadiliko ya teknolojia ikiwemo akili unde (AI), na kuitumia kama nyenzo ya kukuza na kuboresha sekta ya utalii nchini.

Akizungumza leo Septemba 25, 2026 katika Kongamano la nne la kimataifa la utalii Arusha 2026 lililofanyika katika hotel ya Mount Meru, Mhe. Mabula amebainisha kuwa matumizi ya akili unde hayapaswi kuondoa nafasi ya binadamu, bali yatumike kuboresha huduma, kuonesha vivutio, kujua mahitaji ya watalii na kujua usimamizi mzuri wa rasilimali za utalii.

Aidha, Mhe. Mabula amesisitiza kuwa kuutangaza utalii na vivutio vyake kitaifa na kimataifa, haiishii tu kwenye vipeperushi na maonesho pekee, bali simu za mkononi, tovuti na mitandao ya kijamii  inatumika, hivyo, amehimiza umuhimu wa upatikanaji wa taarifa sahihi zinazohusu utalii na vivutio vya utalii nchini kwenye mazingira ya kidijitali.

"Ushindani wetu wa utalii haupo tena kwenye vipeperushi na maonesho ya utalii pekee, bali umehamia kwenye simu, mitandao na mifumo ya AI, hivyo tuhakikishe taarifa za vivutio zinapatikana kwenye mazingira hayo ya kidijitali"  amesema

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Cha Uhasibu Arusha-IAA Prof. Eliamani Sedoyema amesema sekta ya utalii haiwezi kutegemea tu mbinu za asili katika ufanyaji kazi, bali teknolojia ya Akili unde ni muhimu kutumika kusaidia watalii kujua maeneo ya utalii, vivutio, kupokea maoni pamoja na kupata taarifa za utalii kwa wakati kabla ya kufanya safari zao.

Jiyoung Rhee Yoon, Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa kampuni ya Empower Africa, amesema uzoefu wake wa kuona matumizi ya Akili Unde (AI) katika utalii nchini Korea na Marekani unaonesha namna teknolojia hiyo inavyoweza kuboresha huduma, malazi na kukidhi mahitaji ya watalii, hivyo mbinu hizo zinaweza kuigwa na kutumika kuboresha na kubadilisha sekta ya utalii nchini Tanzania.

Kongamano la Kimataifa la Utalii Arusha 2026 (AITC) limefanyika chini ya kaulimbiu "Ajenda ya Kidijitali na Akili Unde katika Kubuni Upya Sekta ya Utalii".


























Post a Comment

0 Comments