Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

WASICHANA MOROGORO KUGEUKIA TEHAMA KUTATUA CHANGAMOTO ZA JAMII



MOROGORO: Wasichana kutoka shule 10 za Mkoa wa Morogoro kesho wanaingia katika Kambi ya Mafunzo (Boot Camp) ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), wakiwa na lengo la kujifunza, kubuni na kutumia teknolojia kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maisha ya kila siku.

Kambi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Kuziba Pengo la Kidijitali: Kuhakikisha Elimu ya Ujuzi wa Kidijitali Inayozingatia Usawa wa Kijinsia kwa Wanawake na Wasichana (Closing the Digital Divide: Ensuring Gender-Transformative Digital Skills Education for Women and Girls), unaotekelezwa na UNESCO kwa ufadhili wa Chuo Kikuu cha Beijing Normal (BNU), kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kabla ya kuanza kwa mafunzo hayo, leo wadau wa mpango huo wamekutana katika Ukumbi wa Odema Hotel, Morogoro, kwa kikao cha maandalizi kilicholenga kuweka mikakati ya kuhakikisha mafunzo hayo yanaacha matokeo yanayoendelea hata baada ya wanafunzi kurejea shuleni.

Mradi huo unalenga kuongeza fursa kwa wasichana kupata ujuzi wa kidijitali, kuwajengea hamasa na uelewa kuhusu masomo na taaluma za TEHAMA, pamoja na kukabiliana na mitazamo ya kijinsia inayoweza kuwafanya wasichana kuona teknolojia kama eneo linalohusishwa zaidi na wavulana.

Miongoni mwa maeneo muhimu ya utekelezaji wa mradi huo ni kuimarisha uwezo wa walimu, kuongeza fursa kwa wasichana kujifunza ujuzi wa kidijitali, pamoja na kuanzisha na kuimarisha Klabu za TEHAMA (ICT Clubs), malezi na ushauri wa kitaalamu (mentorship) na shughuli za ubunifu.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Faith Shayo amesema msisitizo wa mafunzo hayo si kuwapatia wasichana maarifa ya TEHAMA kwa muda mfupi, bali kuwajengea hamasa na shauku ya kuendelea kujifunza na kutumia teknolojia.

Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuwafanya wasichana waone kwamba TEHAMA inaweza kuwa sehemu ya maisha yao, masomo yao na njia ya kutengeneza suluhisho kwa changamoto zinazowazunguka. “Lengo ni kuwajengea hamasa watoto wa kike ili waweze kupenda masomo ya sayansi na kuona uwezo wa TEHAMA katika teknolojia,” amesema Dkt. Shayo.

Amesema jumla ya wasichana 500 wanalengwa kunufaika na mpango huo, huku akisisitiza kuwa Kambi ya Mafunzo ya wiki hii si mwisho wa programu.

Baada ya mafunzo, wanafunzi watarudi katika shule zao na kuendelea na shughuli za Klabu za TEHAMA, huku wataalamu wakiendelea kuzifuatilia shule hizo na walimu pamoja na wakuu wa shule wakitarajiwa kusimamia mwendelezo wa klabu hizo.

Kwa kuzingatia nafasi kubwa ya kilimo katika Mkoa wa Morogoro, wanafunzi watatumia ujuzi watakaoupata kubuni suluhisho linalolenga sekta hiyo.

Miongoni mwa ubunifu unaotarajiwa kuwasilishwa ni Mkulima Mahiri (Smart Farmer), mfumo unaolenga kutumia Akili Bandia (Artificial Intelligence – AI) kumsaidia mkulima kutambua tatizo linaloweza kuikabili mimea.

Kupitia mfumo huo, mkulima ataweza kupiga picha ya mmea kwa kutumia simu, kisha mfumo kuchambua picha hiyo na kumsaidia kubaini tatizo linaloweza kuwa limeathiri mmea.

Ubunifu mwingine utahusu mfumo wa kuripoti matukio na changamoto zinazowakabili wananchi, ikiwemo matatizo ya maji, barabara na huduma nyingine muhimu katika jamii.

Kwa kufanya hivyo, Kambi hiyo inalenga kuwatoa wanafunzi katika nafasi ya kuwa watumiaji wa teknolojia pekee na kuwajengea uwezo wa kuwa wabunifu na watatuzi wa changamoto kupitia TEHAMA.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema Wizara ina jukumu la kuandaa sera na miongozo, lakini utekelezaji wa sera hizo unahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali.

Ameishukuru UNESCO, BNU, wawezeshaji kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) pamoja na viongozi wa shule kwa kushiriki katika mpango huo, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wasichana wanapata fursa sawa za kujifunza na kutumia TEHAMA.

Amesema jamii inapaswa kuacha mitazamo inayoweza kuwafanya watoto wa kike waachwe nyuma katika matumizi ya teknolojia na badala yake kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika masomo ya sayansi na TEHAMA.

Kwa upande wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Eng. Joyce Baravuga, Mratibu wa Mafunzo ya Kidijitali (E-Learning Coordinator), amesema programu hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha elimu ya kidijitali nchini.

Amepongeza wakuu wa shule zilizochaguliwa kushiriki, akisema utayari na uthubutu wa shule ni miongoni mwa mambo yaliyozingatiwa katika uteuzi huo.

Eng. Baravuga amewataka walimu na wakuu wa shule kuwa wadau wakuu wa mpango huo kwa kuhakikisha Klabu za TEHAMA zinaendelea baada ya wanafunzi kurejea shuleni na kwamba maarifa yanayopatikana yanawafikia wanafunzi wengine.

Aidha, amewataka walimu na wawezeshaji kukusanya taarifa za utekelezaji wa shughuli za mradi kila siku ili kuwezesha kupima mafanikio, kubaini mapungufu na kutoa msingi wa kuboresha programu katika hatua zijazo.

Amesisitiza pia umuhimu wa wanafunzi kuchaguliwa kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa bila upendeleo, ili kuhakikisha fursa zinazotolewa zinawafikia walengwa kwa usawa.

Mradi wa Kuziba Pengo la Kidijitali unalenga pia kuongeza uelewa wa walimu, wazazi, viongozi wa shule na jamii kuhusu umuhimu wa ushiriki wa wasichana katika elimu na taaluma zinazohusiana na TEHAMA.

Morogoro ni miongoni mwa maeneo yanayolengwa katika utekelezaji wa shughuli za mradi huo, pamoja na Dodoma.

Kesho, macho yanaelekezwa Shule ya Sekondari Kilakala, ambako wasichana kutoka shule 10 wataanza rasmi Kambi ya Mafunzo, wakibeba si tu matarajio ya kujifunza TEHAMA, bali pia nafasi ya kuonesha kwamba teknolojia inaweza kuwa nyenzo ya kubadili maisha na kutatua changamoto za jamii.

Kwa mradi huu, kuziba pengo la kidijitali hakumaanishi kuwapa wasichana teknolojia pekee, bali kuwapa maarifa, ujasiri na nafasi ya kuitumia teknolojia kuunda mustakabali wao.

Post a Comment

0 Comments