Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

BoT YAENDELEA NA RIBA YA ASILIMIA 6.25 KWA YA NNE 2026

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeamua kuendelea kuweka kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) katika asilimia 6.25 kwa robo ya mwaka inayoishia Desemba 2026, ikisema hatua hiyo inalenga kudhibiti mfumuko wa bei na kuendelea kuchochea ukuaji wa uchumi.

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya Kamati ya Sera ya Fedha kufanya tathmini ya mwenendo wa uchumi wa ndani na dunia, pamoja na vihatarishi vinavyoweza kuathiri mfumuko wa bei na ukuaji wa uchumi.

Tutuba amesema mfumuko wa bei Tanzania Bara unatarajiwa kuendelea kubaki ndani ya lengo la muda wa kati la asilimia 3 hadi 5, licha ya shinikizo linalotokana na kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia, migogoro ya kimataifa na uwezekano wa athari za hali ya hewa ya El Niño.

Amesema mfumuko wa bei Tanzania Bara ulifikia asilimia 4.3 Agosti 2026, kutoka wastani wa asilimia 4.1 katika robo ya mwaka iliyoishia Juni 2026. Ongezeko hilo lilichangiwa zaidi na kupanda kwa bei za mafuta duniani, hali iliyoongeza gharama za usafirishaji na uzalishaji.

Kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa bei ulipungua hadi asilimia 5.6 Agosti 2026, kutoka asilimia 6.0 Julai, ingawa bado ulikuwa juu ya lengo la muda wa kati la asilimia 5.

Katika sekta ya mikopo, BoT imesema mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kukua kwa kasi na kufikia wastani wa asilimia 32.5 katika robo ya mwaka iliyoishia Septemba 2026.

Tutuba amesema ukuaji huo umewezesha wafanyabiashara, kampuni na wananchi kupata fedha kupitia benki kwa ajili ya kuendeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Aidha, BoT imesema sekta ya benki imeendelea kuwa imara na yenye uwezo wa kustahimili changamoto, ikiwa na mitaji, ukwasi na faida ya kutosha. Mikopo chechefu imeendelea kuwa chini ya kiwango kinachokubalika, ikiwa asilimia 2.5 Agosti 2026, dhidi ya ukomo wa asilimia 5.

Kwa upande wa uchumi, BoT inatarajia Tanzania Bara kukua kwa asilimia 6.6 mwaka 2026, huku ukuaji huo ukichangiwa na kuimarika kwa shughuli za kifedha, uzalishaji viwandani, uwekezaji katika miundombinu na huduma za kijamii.

Zanzibar, kwa upande wake, uchumi ulikua kwa asilimia 6.7 katika robo ya kwanza ya 2026, huku ukitarajiwa kukua zaidi ya asilimia 7 katika robo ya pili na ya tatu, kutokana na kuimarika kwa utalii, ujenzi na miradi ya maendeleo.

BoT pia imesema akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kutosha, ikiwa zaidi ya dola bilioni 6, kiasi kinachotosheleza mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa takribani miezi 4.3.

Mkutano ujao wa Kamati ya Sera ya Fedha utafanyika Januari 6, 2027, ambapo uamuzi wa CBR kwa robo ya kwanza ya mwaka 2027 utafanywa, huku uamuzi huo ukitarajiwa kutangazwa Januari 7, 2027.

Post a Comment

0 Comments