Na, Mwandishi wetu- Maputo, Msumbiji
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya akimwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na wenye Ulemavu) Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Kongamano la Usimamizi wa Maafa kuhusu Kupunguza Hatari za Maafa na Kuimarisha Ustahimilivu wa Bara la Afrika dhidi ya majanga linalofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 13 hadi 15 Oktoba, 2026 Jijini Maputo Nchini Msumbiji.
Kongamano hilo limefunguliwa rasmi hii leo (13 Oktoba 2026) na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Daniel Chapo na kueleza kuwa limekuja wakati sahihi na mahali sahihi kwa kuzingatia changamoto za mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha ongezeko la majanga mbalimbali ikiwemo ya ukame, mafuriko, matetemeko ya ardhi, vimbunga vya baharini na mengine mengi.
Ameeleza kuwa ujio wa nchi zote husika kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja kwa majanga ya aina zote ikiwemo ya asili na yale yasiyo ya asili ni hatua muhimu kwa kuzingatia kuwa majanga yanatokea kila mahali lakini madhara hutofautiana kulingana na maandalizi na mipango ya nchi husika katika kukabili maafa.
“Lazima kuwe na mipango imara ya kiuchumi na kijamii katika kukabili maafa, upande wa Msumbiji imeendelea kujithatiti kuhakikisha inakabili maafa na kujiweka tayari, nashukuru uwepo wa Kongamano hilo ambalo limetuleta pamoja ili tuweke mikakati ya kukabiliana na maafa kwa nchi zetu za Afrika, na kuhakikisha tunapunguza madhara yatokanayo na maafa,”alisisitiza
Lengo kuu la Kongamano hilo ni kuchochea mabadiliko ya kimkakati ili kuimarisha uwezo wa kukabiliana na athari za ukame na kupunguza hatari za maafa kwa kuimarisha mifumo ya kiutawala katika usimamizi wa maafa na kuongeza uwekezaji wa kimkakati ili kuimarisha ustahimilivu dhidi ya majanga.
Aidha, Kongamano hilo limekusudia kutoa fursa ya kujadili mikakati ya ugharamiaji wa hatua za mapema, kuweka mikakati thabiti ya kuzuia majanga kabla hayajatokea na kutafuta ufumbuzi wa changamoto za upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya kukabiliana na changamoto zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi na uwekezaji wa muda mrefu.
Vilevile, Kongamano linatarajiwa kushirikisha wadau na sekta mbalimabli ili kuleta pamoja watunga sera, jumuiya za kiuchumi za kikanda, taasisi za kifedha, washirika wa maendeleo, wasomi, sekta binafsi, na asasi za kiraia ili kuwaza kuhakikisha uwajibikaji wa pamoja.
Kongamano hilo limeandaliwa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Msumbiji pamoja na Sekretarieti ya SADC. Kaulimbiu ya Kongamano hilo ni “Kuimarisha Utawala katika Usimamizi wa Maafa na Uwekezaji wa Kimkakati ili kupunguza hatari za Maafa na kujenga Afrika imara inayostahimili majanga"









0 Comments