Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, akizungumza mwakilishi wa mkandarasi wa ujenzi wa Barabara ya Kahama–Bulyanhulu Jct–Kakola, M/s China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) Bw. Wang Lei (Mchina mwenye miwani) , kushoto kwa Waziri , Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Ntuli Mwaikokesya, anayefuata ni Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mabula Magangila na baadhi ya wahandisi wa Mkoa wa Shinyanga.

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, akisoma ramani ya ujenzi wa barabara hiyo ya Kahama- Bulyanhulu Jct-Kakola wakati alipofanya ziara kwenye ujenzi wa barabara hiyo.
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa akizungumza wakati akitembelea ujenzi wa barabara ya Bulyanhulu Jct-Kakola.
***
#Mkandarasi atakiwa kumaliza kazi mapema mwezi ujao.
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, amemtaka Mkandarasi wa ujenzi wa Barabara ya Kahama–Bulyanhulu Jct–Kakola, M/s China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati mapema mwezi ujao kwa mujibu wa mkataba.
Mradi wa ujenzi wa barabara barabara hiyo kwa kiwango cha lami yenye kilomita 73 unatekelezwa kwa uwezeshaji wa migodi ya Barrick nchini inayoendeshwa kwa ubia na serikali kupitia kampuni ya Twiga ya Bulyanhulu na North Mara kwa gharama ya shilingi bilioni 101.2 na umeanza kutekelezwa mwaka juzi kwa usimamizi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS).
Akiongea baada ya kutembelea barabara hiyo amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ili barabara hiyo iweze kumalizika katika muda uliopangwa na kuwaondolea wananchi wanaotumia barabara hiyo kero ya usafiri sambamba na kuwanufaisha wananchi wanaotegemea kuitumia kwa usafirishaji wa bidhaa mbalimbali na kupanua wigo wa ufanyaji wa biashara na kukuza uchumi.
Waziri Kadogosa amesisitiza kuwa mkandarasi anatakiwa kukamilisha mradi huo kwa mujibu wa mkataba ifikapo Desemba 7, 2026, akionya kuwa Serikali itachukua hatua kali endapo atashindwa kutekeleza wajibu wake, ikiwemo kukata asilimia 0.1 ya thamani ya mkataba na kufuta kibali cha kampuni hiyo kutekeleza miradi ya aina hiyo nchini.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Ntuli Mwaikokesya, amesema ujenzi wa barabara ya Kahama – Bulyanhulu Jct–Kakola wenye urefu wa kilomita 73 unagharimu Shilingi bilioni 100.6.

Amesema mradi huo ulipangwa kukamilika mwezi Septemba 2026, hata hivyo, kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji, mkandarasi aliomba kuongezewa muda wa kukamilisha kazi na mpaka sasa kilomita 32 kati ya 73 zimekamilishwa kwa kuwekwa lami, huku kazi nyingine za ujenzi zikiendelea katika maeneo mbalimbali ya mradi.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mhe. Mabula Magangila, amesema wananchi wamekuwa na uhitaji wa muda mrefu wa barabara hiyo, akibainisha kuwa kukamilika kwake kutachochea shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.
Mwakilishi wa Mgodi wa Barrick ambao ndiyo wafadhili wa Ujenzi wa Barabara hiyo kwa asilimia 100, Mhandisi Ibrahim Paul ameunga mkono kauli ya Waziri Kadogosa kwa kumtaka mkandarasi kumaliza kazi kwa wakati kwa kuwa fedha za uwezeshaji zinatoka kwa wakati mkandarasa akihitaji kulipwa na kuwa Barrick inapenda kuona dhamira yake ya kuona wananchi wananufaika na mradi huo ikitimia.
Mhandisi Bw. Wang Lei kutoka kampuni ya CCECC inayojenga barabara hiyo ameahidi kuongeza juhudi na kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa.Kukamilika kwa barabara hii ambayo ilianza kujengwa mnamo mwezi Julai mwaka juzi kutafungua fursa za kiuchumi za madini, Kilimo, Misitu na Utalii katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Tabora, Kagera na Kigoma.
Pamoja na Barabara hiyo kufungua fursa za kiuchumi za madini, kilimo, misitu na utalii katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Tabora, Kagera na Kigoma mara baada ya kukamilika pia barabara hiyo ni muhimu katika shughuli za kiuchumi na kijamii kwa Mkoa wa Shinyanga hususani Manispaa ya Kahama ambako kuna mkusanyiko mkubwa wa Wasafirishaji wa mizigo kutoka bandari kuu ya Tanzania kwenda nchi za jirani za Rwanda na Uganda.
Mkakati endelevu wa kampuni ya Barrick ambayo inawezesha ujenzi huo unabainisha kuwa Uchimbaji madini ukifanyika kwa umahiri ni nguvu kubwa ya kuleta maendeleo na jamii zinazoishi kwenye maeneo ya shughuli zake zikipata mafanikio ni mafanikio yake pia.























0 Comments