Na Mwandishi Wetu.
Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Kampasi ya Mwanza, imeendelea kuimarisha ushirikiano na jamii kwa kusaidia kutatua changamoto za elimu katika Shule ya Sekondari Kilimani, Wilaya ya Ilemela, kupitia msaada wa mashine ya Printer/Photocopy yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 3, itakayorahisisha uchapishaji wa mitihani na nyenzo za kujifunzia.
Akizungumza katika Mahafali ya 12 ya Kidato cha Nne ya shule hiyo, tarehe 6 Novemba 2026, Kaimu Mkurugenzi wa DIT Mwanza, Ndugu William Lohay, amesema Serikali kupitia wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 37 kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, maabara na karakana za kisasa, hivyo kuwataka wazazi kuwaleta vijana wao DIT kunufaika na fursa za elimu ya Sayansi na Teknolojia.
Ameongeza kuwa DIT itaendelea kushirikiana na shule hiyo, ikiwemo kusaidia wanafunzi wao kuja DIT na kutumia maabara ya kompyuta na walimu wa TEHAMA ili kuwapa fursa wanafunzi wao kujifunza kwa vitendo zaidi masomo hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Lutaro Dallu, ameishukuru DIT kwa msaada huo akisema, “Mashine hii itapunguza gharama za uchapishaji na kurahisisha maandalizi ya mitihani, tofauti na awali ambapo tulilazimika kuchangisha fedha kutoka kwa wanafunzi.”
Naye mwanafunzi Michael Mathew, kwa niaba ya wenzake Sarah Leonard na Flora Japhali, amesema, “Msaada huu utaturahisishia kupata mitihani ya mazoezi mara kwa mara na kuboresha maandalizi yetu ya kitaaluma.”
Hatua hiyo inaonesha dhamira ya DIT Mwanza katika kuimarisha uwajibikaji kwa jamii (Corporate Social Responsibility), kukuza ushirikiano na taasisi za elimu na kuweka mazingira bora ya ujifunzaji kwa vijana, sambamba na kuendeleza wataalamu wenye ujuzi katika Sayansi na Teknolojia.









0 Comments