Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

EWURA KUPITIA UPYA BEI ZA CNG BAADA YA MIAKA 15


MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeanza mchakato wa kupitia upya bei za Gesi Asilia Iliyokandamizwa (CNG) inayotumika kwenye magari, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha bei hizo zinaendana na gharama halisi za uendeshaji, uwekezaji na uwezo wa wananchi kumudu huduma hiyo.

Mapitio hayo yanakuja baada ya kubainika kuwa bei za CNG zimeendelea kubaki katika viwango vilevile kwa takribani miaka 15, licha ya mabadiliko ya gharama katika mnyororo wa uzalishaji, usafirishaji, uhifadhi na usambazaji wa gesi asilia.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, katika semina ya wadau kuhusu usalama wa matumizi ya CNG, Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki, Lorivii Lon'gidu, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Salum Mnuna, alisema EWURA imeamua kukusanya maoni ya wadau kuhusu mapendekezo ya viwango vya faida na bei kikomo za nishati hiyo.

Alisema ushirikishwaji wa wadau ni muhimu katika kuhakikisha maamuzi yatakayofikiwa yanazingatia maslahi ya pande zote, wakiwemo wawekezaji, watoa huduma na wananchi wanaotumia gesi hiyo.

“Tunapenda kuona maoni yenu na ushauri wenu kuhusu mapendekezo ya viwango vya faida na bei kikomo za CNG, ili sisi kama wadhibiti tuyazingatie na kuhakikisha shughuli hizi zinafanikiwa kwa njia salama zaidi,” alisema.

Kwa upande wake, Meneja wa Mitambo ya Gesi Asilia wa EWURA, Selemani Chombo, alisema mapitio hayo yanazingatia gharama za uendeshaji, mabadiliko ya thamani ya fedha za kigeni pamoja na gharama za kusafirisha gesi hiyo kwenda katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema kwa sasa bei ya CNG jijini Dar es Salaam ni Sh1,550 kwa kilo, lakini kuongezeka kwa matumizi ya nishati hiyo na kusambaa kwa huduma katika maeneo ya Morogoro, Kibaha, Mtwara na Ruvuma kunahitaji mfumo wa bei unaozingatia gharama za kufikisha huduma katika kila eneo.

Alifafanua kuwa umbali kutoka kwenye chanzo cha gesi pamoja na gharama za usafirishaji ni miongoni mwa mambo yanayoweza kusababisha tofauti ya bei kati ya eneo moja na jingine.

Chombo alisema EWURA itazingatia sheria na kanuni zilizopo katika mchakato huo, huku wazalishaji, watoa huduma na watumiaji wakipewa nafasi ya kutoa maoni kabla ya viwango vipya vya bei kutangazwa na kuanza kutumika rasmi.

Aliongeza kuwa lengo ni kuweka uwiano kati ya maslahi ya wafanyabiashara na watumiaji, ili wawekezaji waweze kuendesha shughuli zao kwa uendelevu huku wananchi wakiendelea kupata huduma hiyo kwa gharama wanazoweza kumudu.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tembo Energies Limited, Prasanna Kumar, alisema matumizi ya gesi asilia kwenye magari yanaendelea kuwa mkombozi kwa wananchi, hasa wakati bei za petroli na dizeli zinapopanda kutokana na changamoto za uchumi wa dunia na vita vya Mashariki ya Kati.

Alisema kampuni hiyo, ambayo ni ya kwanza inayomilikiwa na Watanzania kuendesha kituo mama cha gesi asilia, imehudumia wananchi jijini Dar es Salaam kwa takribani miezi 26, huku katika vipindi vya mahitaji makubwa ikiweza kuhudumia zaidi ya magari 1,000 kwa siku.

Kumar alisema licha ya gharama kubwa za uwekezaji na viwango vidogo vya faida kwa waendeshaji, anaunga mkono kuendelea kuwa na bei tulivu ili kuhamasisha wananchi wengi zaidi kutumia nishati hiyo.

Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa Serikali kuweka uwazi katika mfumo wa kupanga na kutoza bei za gesi, akipendekeza mikataba na malipo ya gesi yafanyike moja kwa moja kwa shilingi za Tanzania badala ya kutegemea thamani ya Dola za Marekani, ili watumiaji waweze kuelewa gharama wanazolipia.

Kuhusu upanuzi wa huduma hiyo, alisema Tembo Energies inaandaa mradi wa kituo kidogo cha gesi asilia iliyoyeyushwa mkoani Mtwara, utakaosaidia kusambaza gesi katika mikoa ya Dodoma, Mwanza na Mbeya.

Kwa upande wake, Mkaguzi wa Masuala ya Usalama wa Gesi Asilia, Baraka Majengo, alisema semina zinazoratibiwa na EWURA zinaongeza uelewa wa wadau kuhusu ubora na usalama wa matumizi ya gesi hiyo.

Alisema suala la usalama ni muhimu zaidi kwa kuwa CNG inatumika katika magari yanayosafirisha abiria, hivyo elimu na uzingatiaji wa taratibu za usalama ni muhimu katika kulinda maisha ya wananchi.

Post a Comment

0 Comments