SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) linatarajia kuadhimisha Siku ya Viwango Duniani mwaka 2026 kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa viwango, sambamba na kutoa tuzo kwa wadau waliochangia kuimarisha ubora na usalama wa bidhaa na huduma nchini.
Maadhimisho hayo yanalenga kutambua mchango wa wadau katika kukuza utamaduni wa kuzingatia viwango, pamoja na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu nafasi ya viwango katika kuhakikisha matumizi ya bidhaa salama na zenye ufanisi, hususan vifaa vinavyotumia nishati.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 24, 2026, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uandaaji Viwango wa TBS, Dkt. Candida Shirima, amesema maadhimisho hayo yatakuwa fursa ya kukutana na wadau mbalimbali, kutoa elimu kuhusu viwango na kutambua wale wanaoshiriki katika kuimarisha ubora nchini.
Amesema katika maadhimisho hayo, TBS itatoa tuzo maalumu kwa viongozi wanaosimamia kamati za kitaalamu za uandaaji wa viwango vya kitaifa, pamoja na wafanyabiashara na watoa huduma walioshiriki na kushinda Tuzo za Ubora za mwaka 2026.
Ameeleza kuwa tuzo hizo zinalenga kutambua juhudi na mchango wa wadau hao katika kuzingatia viwango, huku zikitumika kama chachu ya kuwahamasisha wengine kuweka mbele ubora na usalama katika uzalishaji na utoaji huduma.
Dkt. Shirima amesema TBS itaweka msisitizo katika kutoa elimu kuhusu viwango vya vifaa vinavyotumika katika nishati safi na nafuu, ikiwemo kuwasaidia wananchi kutambua vifaa vinavyotumia nishati kwa ufanisi ili kupunguza matumizi ya umeme.
Amesema suala hilo linaendana na kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo “Maono ya Pamoja kwa Dunia Bora: Nishati Nafuu na Safi kwa Wote,” inayosisitiza umuhimu wa viwango katika kuhakikisha bidhaa za nishati zinakidhi mahitaji ya ubora, usalama na ufanisi.
Aidha, amesema TBS tayari imeandaa viwango vya bidhaa zinazotumika katika nishati safi ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ulioanzishwa kwa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesisitiza kuwa kupitia maadhimisho hayo, TBS inalenga kuunganisha juhudi za wadau katika kuendeleza matumizi ya viwango, kuimarisha ubora wa bidhaa na huduma na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za nishati safi na nafuu nchini.
0 Comments