Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

TBS YAWATAKA WAZALISHAJI WA VIFAA VYA NISHATI JADIDIFU KUZINGATIA VIWANGO VYA UBORA

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewahimiza wazalishaji wa bidhaa na vifaa vinavyotumia nishati jadidifu kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi matakwa ya viwango vya ubora na usalama ili kuongeza ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi.

Wito huo umetolewa na Afisa Masoko Mwandamizi wa TBS, Rhoda Mayungu, wakati shirika hilo liliposhiriki katika maonyesho ya Wiki ya Nishati Jadidifu (Renewable Energy Week), yenye lengo la kutoa elimu kwa wazalishaji kuhusu umuhimu wa viwango katika uzalishaji wa bidhaa za nishati.

Mayungu amesema bidhaa zinazothibitishwa na TBS huongeza imani kwa watumiaji, huku zikimuwezesha mzalishaji kupanua wigo wa soko na kuuza bidhaa zake katika soko la ndani na Jumuiya ya Afrika Mashariki bila vikwazo vinavyotokana na kutokidhi matakwa ya viwango.

Aidha, amesema TBS ina maabara za kisasa zinazotumika kupima ubora na ufanisi wa bidhaa zinazohusiana na nishati, ambazo pia zinatoa fursa kwa wazalishaji na watumiaji kujiridhisha kuhusu ubora na utendaji wa vifaa wanavyovitumia.

Amesisitiza kuwa wazalishaji wa nishati wanapaswa kutumia maabara hizo kupima vifaa vyao ili kuhakikisha nishati inayozalishwa inakidhi matumizi yaliyokusudiwa na kuwa salama kwa watumiaji.

Katika hatua nyingine, Mayungu amewahimiza wajasiriamali wadogo na wa kati kutumia fursa ya huduma ya uthibitishaji wa bidhaa inayotolewa bure na TBS kwa kundi hilo, akieleza kuwa wanachotakiwa ni kupata barua ya utambulisho na kuwasilisha bidhaa zao kwa ajili ya kuthibitishwa.

Amesema ushiriki wa TBS katika maonyesho hayo umekuwa muhimu kwa kuwawezesha kuwafikia wazalishaji moja kwa moja, kutoa elimu ya viwango na kutatua changamoto zinazohusiana na uthibitishaji wa bidhaa, huku akieleza kuwa mapokezi yamekuwa mazuri na kuongeza uelewa wa wadau kuhusu nafasi ya TBS katika sekta ya nishati jadidifu.

Post a Comment

0 Comments