NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha vijana wa kizazi cha Gen Z katika mijadala ya maamuzi na maendeleo ya Afrika, kikieleza kuwa kundi hilo lina nafasi kubwa ya kuchochea maendeleo ya bara hilo endapo litapewa fursa na mazingira sahihi ya kutumia uwezo wake.
Akizungumza kuhusu matokeo ya mkutano wa kitaaluma wa The Voice of Social Sciences 2026, uliofanyika kwa siku mbili, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Ndaki ya Sayansi za Jamii ya UDSM na mmoja wa waandaaji wa mkutano huo, Richard Sambaiga, amesema majadiliano yaliyofanyika yameangazia nafasi ya vijana wa Gen Z kama wadau muhimu katika harakati za kijamii na mabadiliko barani Afrika.
Sambaiga amesema mjadala umeonesha kuwa vijana wanapaswa kutazamwa kama chachu ya kufanikisha Ajenda ya Afrika 2063, inayolenga kujenga Afrika inayotakiwa, kwa kuwa ni sehemu muhimu ya nguvu kazi na injini ya maendeleo ya bara hilo.
Hata hivyo, amesema vijana wanaweza pia kuwa changamoto kwa maendeleo ya Afrika endapo matarajio, mahitaji na matamanio yao hayatashughulikiwa ipasavyo, akieleza kuwa wanaweza kuwa wajenzi wa maendeleo au kuchangia kuyadumaza kulingana na namna jamii inavyowashirikisha na kuwaandaa.
Amesema jukumu la kuwawezesha vijana halipaswi kuachwa kwa kundi hilo pekee, bali linahitaji ushirikiano wa taasisi za elimu, serikali na sekta mbalimbali katika kuhakikisha wanapata fursa na mazingira yatakayowawezesha kutumia uwezo wao na kutimiza matarajio yao.
Amesema, vyuo vikuu vina wajibu wa kuwaandaa vijana kupitia elimu na maarifa yatakayowawezesha kutumia fursa zilizopo, huku serikali na sekta nyingine zikihitaji kuweka mifumo inayowapa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Amesema katika majadiliano hayo, vijana wameeleza kutaka kuwa sehemu ya mijadala na michakato ya kufanya maamuzi badala ya kuachwa pembeni huku watu wengine wakiwafanyia maamuzi, pamoja na kutaka kupata fursa zitakazowawezesha kuboresha maisha yao na jamii kwa ujumla.
Aidha, amesema vijana wanahitaji mazingira ambayo yatawezesha mawazo na maoni yao kusikilizwa na kueleweka bila kutafsiriwa kama nia ya kuharibu mustakabali wa Afrika.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa kizazi cha watu wazima kujifunza kuwaelewa vijana, huku vijana nao wakijenga utayari wa kuelewa mitazamo ya vizazi vingine ili kuimarisha mshikamano na kuishi pamoja kwa maelewano.
Amesema mkutano huo umekuwa na tija kwa kuwa umewezesha watafiti kuchambua changamoto zinazolikabili kundi la Gen Z, kujadili nafasi yao katika jamii na kutoa mapendekezo ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha vijana wanakuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za maendeleo ya Afrika.

















0 Comments