Ticker

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA YAKAGUA MAENDELEO YA MAFUNZO YA UANAGENZI NA MIRADI ILIYOZINDULIWA NA MBIO MAALUM ZA MWENGE WA UHURU MKOANI SINGIDA

Na: Mwandishi Wetu – Singida

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imetembelea na kukagua miradi inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwemo Mafunzo ya Uanagenzi yanayotolewa kwa vijana kupitia Vyuo vya Ufundi stadi mbalimbali vilivyopo nchini pamoja na kukagua miradi iliyozinduliwa na mbio maalumu za Mwenge wa Uhuru katika Mkoa wa Singida.

Kamati hiyo iliyoongozwa na Makamu Mwenyekiti wake Mhe Najma Giga (Mb.) imetembelea Chuo Cha VETA na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu ambavyo vinatoa mafunzo ya uanagenzi kwa vijana. Pia kamati hiyo imetembelea Maabara ya Mafunzo ya Kompyuta, Karakana ya Umeme katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi, Ofisi ya udhibiti wa Ubora wa Elimu na mradi wa maji uliopo Nguka Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida, miradi hiyo ilizinduliwa wakati wa mbio maalum za mwenge wa Uhuru.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe Najma Giga (Mb.) alieleza kuwa kamati hiyo imekuwa ikisimamia miradi mbalimbali inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na wameridhishwa namna ofisi hiyo imekuwa ikitekeleza mambo mbalimbali ambayo yamekuwa yakishauriwa na kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria.

“Tumefurahi kuona mafunzo haya ya Uanagenzi wanayopatiwa vijana wakiume, wakike na wenye ulemavu kupitia ufadhili wa Serikali yao yamewasaidia kupata fani mbalimbali za ufundi stadi ambazo zitawasaidia kukuza ujuzi na kuwawezesha waondokane na tatizo la ajira na hivyo kuwawezesha kujiajiri na kuajiri wenzao,” alisema Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe Najma Giga (Mb.)

Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga alisema kuwa Mafunzo hayo ya Uanagenzi yanayoratibiwa na ofisi hiyo awamu ya tatu ilianza rasmi Juni 2021 katika mikoa yote ya Tanzania Bara ambapo jumla ya vyuo 72 vinashiriki kutoa mafunzo hayo.

“Hadi sasa jumla ya Vijana 14,440 wamenufaika na mafunzo ya Uanagenzi na mafanzo hayo yanagharamiwa na serikali kwa asilimia 100 kupitia fedha zilizopitishwa na Bunge letu Tukufu kwa lengo la kuwasaidia vijana ambao ndio nguvukazi ya taifa kupata ujuzi stahiki utakaowawezesha kujiajiri, kuajiri wenzao ama kuajiriwa,” alisema Naibu Waziri Ummy

Alifafanua kuwa Mkoa wa Singida fursa hiyo ya mafunzo ya Uanagenzi imetolewa kwa vijana 395 ikiwa ni sawa na asilimia 91.9, vijana ambao hawajaripoti ni 35 ikiwa ni saw ana asilimia 8.1 ambapo jumla ya vijana 430 walipaswa kupatiwa mafunzo hayo kwa lengo la kuhakikisha fursa zilizotolewa kwa mkoa wa singida hazipotei.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Ng’wasi Kamani (Mb.) alitoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali na waachane na dhana ya kufikiria kuwa mafanikio yanapatikana kwa njia rahisi au kupitia “connection”.

“Ninawasihi vijana wanaopatiwa mafunzo haya ya Uanagenzi watakapo maliza mafunzo yao wachangamkie fursa ya mikopo inayotolewa na halmashauri pamoja na mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ili waweze kuanzisha miradi ya kuichumi,” alisema

Akitoa neno la Shukrani Mnufaika wa Mafunzo hayo ya Unangenzi Bi. Elizabeth Charles ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendelea kukumbuka vijana na kundi la Watu wenye Ulemavu kwa kuwapatia ujuzi ambao utawasaidia kuanzisha shughuli zao binafsi za uzalishaji mali.


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga (katikati) Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe Najma Giga (wa tatu kutoka kushoto) wakisikiliza maelezo ya kijana Idd Ramadhani mnufaika wa mafunzo ya Uanagenzi fani ya Umeme katika Chuo cha VETA wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ya kukagua miradi inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Mkoani Singida.


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe Najma Giga (wa tano kutoka kushoto) akiwa pamoja na wajumbe wa kamati hiyo wakiangalia zulia walipotembelea vikundi vya Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu waliowezeshwa na Mikopo ya Asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kupitia mapato ya ndani wakati wa ziara yao Mkoani Singida.


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga (wa pili kutoka kushoto) Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe Najma Giga (wa tano kutoka kushoto) wakisikiliza maelezo ya vijana wanufaika wa mafunzo ya Uanagenzi fani ya Ufundi Bomba katika Chuo cha VETA Mkoani Singida.


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe Najma Giga akiwa pamoja na wajumbe wa kamati hiyo wakiangalia bidhaa za nguo na mapazia yanayotengenezwa na vijana wenye ulemavu walipotembelea Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu Sabasaba Mkoani Singida kwa lengo la kukagua maendeleo ya Mafunzo hayo.


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe Najma Giga (Mb.) akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua Mafunzo ya Uanagenzi yanayotolewa kwa vijana kupitia Vyuo vya Ufundi stadi mbalimbali vilivyopo nchini pamoja na kukagua miradi iliyozinduliwa na mbio maalumu za Mwenge wa Uhuru katika Mkoa wa Singida. Kulia ni Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Mhe. Kirumbe Ng'enda.


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga akifafanua jambo kuhusu mafunzo ya Uanagenzi yanayoratiwa na Ofisi hiyo wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ya kukagua miradi inayosimamiwa na Ofisi hiyo. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Jamal Katundu.

PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU

(SERA, URATIBU, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)

Post a Comment

0 Comments