Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAWAHIMIZA VIJANA KUTUMIA TEHAMA KUKAMATA FURSA

Na Prisca Ulomi, WMTH, Dar es Salaam



Serikali imewahimiza vijana wa Tanzania kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kukamata fursa zilizopo nchini katika Sekta ya Mawasiliano.



Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mulembwa Munaku wakati akifungua Kongamano la Kidijitali la Vijana Tanzania kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile lililofanyika Dar es Salaam leo



Munaku amesema kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi na rafiki ya kuendeleza na kufanikisha matumizi ya TEHAMA nchini ambapo Wizara hiyo imetengeneza sera ya Taifa ya TEHAMA; sheria na kanuni; ujenzi wa miundombinu ya TEHAMA ikiwemo Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye urefu wa kilomita 8,319 unaofikisha huduma za mawasiliano kwenye mikoa na nchi jirani



Ameongeza kuwa zaidi ya asilimia 75 ya watanzania ni vijana ambapo Serikali imetambua hilo hivyo imeweka mikakati na miradi ya TEHAMA inayogusa vijana ili kuongeza wigo wa fursa za TEHAMA kwa vijana katika nyanja mbali mbali ikiwemo fursa ya ajira; biashara; mafunzo; na ubunifu ili TEHAMA itumike kutatua na kujibu changamoto zilizopo kwenye jamii



Amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021, Serikali imepata mkopo nafuu wa dola za kimarekani milioni 150 kutoka Benki ya Dunia ili kutekeleza mradi wa Tanzania ya Kidijitali ambapo mradi huo utagusa vijana na TEHAMA katika nyanja ya kiuchumi na kijamii



Naibu Kiongozi wa Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Emilio Rossetti amesema kuwa kupitia umoja wao wamekuwa wakitoa misaada nchini na kushirikiana na Serikali kuendeleza na kuongeza matumizi ya TEHAMA nchini hususan kwa vijana na wanawake na wako tayari kuendelea kufanya hivyo ili vijana wanufaike na fursa za TEHAMA zilizopo



Naye Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya DOT Tanzania, Diana Ninsiima amesema kuwa kampuni hiyo imeshirikiana na wadau wengine kuandaa Kongamano hilo ili litumike kama jukwaa la kujenga uelewa kwa jamii kuhusu nafasi ya vijana katika TEHAMA ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni, “Ujuzi wa Kidijitali kwa ajili ya Ajira na Ujasiriamali kwa Vijana,”.



Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mtabe Innovations, Given Edward, akizungumza kwa niaba ya vijana wenzake amesema kuwa hivi sasa vijana wa kitanzania wanapata mazingira sawa na vijana wengine duniani kutumia TEHAMA kuendesha maisha yao na wanaishukuru Serikali kwa kubadilisha mitazamo ya jamii kuhusu umuhimu na manufaa ya TEHAMA kwa vijana na kuongeza ushiriki wa vijana katika TEHAMA



Kongamano hilo limehudhuriwa na wadau mbali mbali waliokuwep ukumbini na wengine kwa njia ya mtandao wakiwemo kutoka Umoja wa Mawasiliano Duniani; Ofisi za ubalozi wa Canada, Ireland; UNICEF; Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia; na kampuni za TEHAMA za vijana zilizopo nchini Tanzania.



Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari




Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mulembwa Munaku akifungua Kongamano la Kidijitali la Vijana Tanzania kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile (hayupo pichani) lililofanyika Dar es Salaam


Naibu Kiongozi wa Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Emilio Rossetti (kushoto) akisikiliza kwa makini mjadala kuhusu Kongamano la Kidijitali la Vijana Tanzania lililofanyika Dar es Salaam. Pembeni yake ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mulembwa Munaku akimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile


Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya DOT Tanzania, Diana Ninsiima akizungumza na washiriki (hawapo pichani) kuhusu Kongamano la Kidijitali la Vijana Tanzania lililofanyika Dar es Salaam


Meneja Mradi na Uendeshaji wa taasisi ya Unleash Africa, Catherine Nyakamo akichangia mada wakati wa Kongamano la Kidijitali la Vijana Tanzania lililofanyika Dar es Saalam


Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mtabe Innovations, Given Edward akizungumza kwa niaba ya vijana (hawapo pichani) kwenye Kongamano la Kidijitali la Vijana Tanzania lililofanyika Dar es Salaam


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Samson Mwela akifafanua jambo kwa washiriki (hawapo pichani) wa Kongamano la Kidijitali la Vijana Tanzania lililofanyika Dar es Salaam


Baadhi ya vijana wakifuatilia mjadala wakati wa Kongamano la Kidijitali la Vijana Tanzania lililofanyika Dar es Salaam


Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mulembwa Munaku (wa tatu kulia), aakimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile, akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wakati wa Kongamano la Kidijitali la Vijana Tanzania lililofanyika Dar es Salaam

Post a Comment

0 Comments