Ticker

6/recent/ticker-posts

‘TUMIENI DHANA YA KAIZEN KUJIKWAMUA KIUCHUMI’ - OLE NASHA


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. William Tate Ole Nasha akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la kaizen Barani Afrika kwa mwaka 2021 linalofanyika leo katika hoteli ya Hyatt Regency, Jijini Dar es salaam.

************************************

Serikali imewataka Watanzania kufuata dhana ya Kaizen katika shughuli zao ili kuongeza ubora na tija ya uzalishaji kwa kusimamia vyema rasilimali watu, kutunza na kutumia muda vizuri, kutumia vizuri maliasili na miundombinu iliyopo ili kuleta tija kwa Taifa na Afrika kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la kaizen Barani Afrika kwa mwaka 2021 linalofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency, Jijini Dar es salaam, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. William Tate Ole Nasha amesema ni heshima kubwa Tanzania kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kwa mwaka huu na kuwataka wajumbe watumie fursa hiyo kujifunza zaidi dhana ya Kaizen ili waweze kuisambaza kwa Wanzania wote.

“Kuweni mabalozi, falsafa zote duniani huenezwa kwa vitendo sio maneno, tumieni nafasi hii kuielewa zaidi ili muweze kuwasaidia wengine kwa mifano ya dhana hii ambayo bado ni ngeni kwenye nchi yetu. Angalieni mfano wa Japan ambayo ni muasisi wa dhana hii pamoja na baadhi ya nchi barani Afrika zimefanikwa kupiga hatua kiuchumi. Vipo vitu kama muda, nafasi, miundombinu na rasilimali mbalimbali ambavyo ninyi mnaviona vya kawaida lakini wenzenu wamevitumia vizuri na wamefanikiwa kiuchumi,” amehimiza Mhe. Ole Nasha.

Aidha, Mhe. Ole Nasha alisema Serikali ya Tanzania ni muumini wa dhana ya Kaizen hiyo, na kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jiansia Wazee na Watoto pamoja na Taasisi zilizipo chini ya Wizara hizo zimeamua kuunda mifumo inayoendeleza dhana hii katika kuhakikisha inaoanishwa na sera mbalimbali za nchi ili kuendeleza jitihada za Serikali za kuleta maendeleo.

“Kazi kubwa ya Serikali ni kuweka mazingira wezeshi ya sera bora na miongozo kwa kushirikiana na wadau wetu ili kuwawezesha wananchi kutumia miongozo hiyo katika utekelezaji. Tumeanza kurekebisha baadhi ya sera na miongozo kama Sera ya Taifa ya Kumlinda Mlaji, Sera ya Taifa ya Haki Miliki na Sera ya Taifa ya Ubora hatimaye kuhakikisha ustawi endelevu wa sekta ya viwanda”, amesema Mhe Ole Nasha.

Katika ufunguzi wa kongamano hilo pia aikuwepo Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Jokate Mwegelo ambaye alisema amefurahi kuwepo hapo kwani imekuwa fursa ya kujifunza na kwamba amefurahishwa na jinsi dhana ya Keizen inavyoweza kutumiwa na watu wa ngazi zote na kuleta matokeo chanya hata yeye angependa kuipeleka elimu hiyo kwa wakazi wa Temeke.

“Wilaya ya Temeke ina wafanyabiashara wengi na biashara ndio tegemeo la uchumi kwa wakazi hao, naangalia falsafa hii itawezaje kuwasaidia wafanyabiashara hao, waweze kuzalisha bidhaa zenye ubora na kupata soko la kitaifa na kimataifa. Nitaomba ushirikiano wenu ili kuwasaidia wakazi wa Wilaya yangu ambao wanajihusisha na shughuli mbalimbali za uchumi ikiwemo viwanda na biashara”, amesema Mhe Jokate.

Mhe.Jokate ameongeza kwamba Serikali inatoa pesa nyingi kuwasaidia wakazi wa Wilaya ya Temeke ili wajikwamue kiuchumi, ikiwa watapatiwa ufahamu wa jinsi dhana ya Kaizen inavyoongeza tija itawainua wakazi wa eneo hilo kufikia viwango vya kimataifa. Aidha, Mhe.Jokate ametumia wasaa huo kumuomba Mhe. Ole Nasha awatembelee wakazi wa Temeke ili kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazoendelea wilayani hapo.

Kongamano la Kaizen Barani Afrika hufanyika kila mwaka ambapo kwa mwaka huu 2021 limeandaliwa na Tanzania na limehudhuriwa na nchi wanachama 16 ambazo zimeshiriki kwa njia ya mtandao. Kauli mbiu ya Kongamano hilo ni Fursa za Kuongeza Kasi ya Maendeleo ya Viwanda na Biashara Afrika; Kuimarisha Kaizen (Ubora Tija) kwa Kutumia Teknolojia ya Kidigitali, Biashara Changa, Maendeleo ya Viwanda na Biashara Ndogo na za Kati pamoja na shughuli za Kiuchumi zenye asili ya Kiafrika.

Post a Comment

0 Comments