Ticker

6/recent/ticker-posts

Steve Nyerere - Watanzania jitokezeni kuchanja kwa hiari Uviko 19



Na Richard Mrusha


Taasisi ya Wazalendo kwanza imewahimiza Watanzania kujitokeza kwa hiari kupata chanjo ya uviko 19, huku ikiwasisitiza kuachana na taarifa za upotoshaji zinazoenezwa na baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa kupitia mitandao ya kijamii kuwa chanjo hiyo ina madhara kwa binadamu.

Hayo yameelezwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa taasisi hiyo Steve Nyerere, ambaye pia ni balozi wa Wizara ya Afya katika mapambano dhidi ya Ugonjwa huo wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es saalam. 

Amesema baadhi ya wanasiasa wamekua wakiwashawishi Watanzania kupitia mitandao ya kijamii wasiende kuchanjwa kwa hiari hali ambayo inasababisha kupoteza uzalendo katika kukabiliana na janga hilo.

" Wapo wanaotumika kisiasa kuhimiza wenzao wasichanje, kama wewe hauchanji acha watu watumie uhuru wao wa kuchanja au kutokuchanja, sisi Wazalendo kwanza tumechanja tunahimiza wale wanaowashawishi Watanzania wasichanje kwa hiari yao waacha tabia hiyo" amesema. 

Ameongeza, "tusitumie mitandao yetu ya kijamii kupotosha jamii, mataifa yaliyoendelea yanatumia mitandao ya kijamii kutangaza mambo muhimu kwa taifa lao ikiwemo Sera za Uchumi".

 Steve ambaye pia ni msanii wa filamu na mchekeshaji maarufu nchini, ameongeza kuwa,  Rais Samia Suluhu Hassan, alijitokeza kuonyesha uzalendo wa kuchanja, hivyo Watanzania wakiwemo vijana na viongozi mbalimbali wajitokeze kwa hiari kuchanjwa ili wajiweke salama kwa afya zao.

Kwa upande wake Mwigizaji wa filamu nchini, Abdalah Mkumbila 'Mhogo Mchungu' aliwashauri Watanzania kuendelea kuchukua hatua za tahadhari kwani Ugonjwa wa Uviko 19 upo na kwamba kundi la watu wenye umri wa kuanzia miaka 50 ndilo lipo katika hatari zaidi .

" Jitetee mwenyewe kwanza halafu na watu wakutetee,tunaomba Watanzania mjitokeze kwa hiari kupata chanjo, ili taifa liwe na maendeleo lazima wananchi wake wawe wazima" amesema. 

Taasisi ya Wazalendo kwanza imekua mstari wa mbele katika kuhimiza Watanzania hususani vijana kuwa wazalendo katika kuunga mkono jitihada za serikali za kuwaletea maendeleo wananchi wake.


Post a Comment

0 Comments