Ticker

6/recent/ticker-posts

IGP SIRRO AWATAKA ASKARI KUONYESHA UWEZO WA MAFUNZO WALIYOYAPATA


***********************************

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro amewataka askari wa Jeshi la Polisi nchini kuonyesha uwezo walioupata kutokana na mafunzo waliyoyapata kwa ajili ya kuwahudumia watanzania na kwa kutenda haki kwa wananchi watakaowahudumia.

IGP Sirro amesema hayo leo wakati wa hafla ya kufunga mafunzo kwa ngazi ya Mkaguzi Msaidizi wa Polisi ambapo wahitimu hao wametakiwa kuhakikisha wanapunguza mrundikano wa mahabusu na kuharakisha upelelezi wa kesi mbalimbali pindi watakaporudi kwenye maeneo yao ya kazi.

Mgeni Rasmi kwenye kufunga mafunzo hayo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Khamis Chilo amewataka askari waliopandishwa vyeo na kuwa Wakaguzi Wasaidizi wa Polisi kufanya kazi kama walivyofundishwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi.

Naye Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo amesema kuwa, vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kuwa pamoja ili kukabiliana na adui atakayejitokeza na kuwataka askari kuwa makini na kutekeleza majukumu yao bila kutengana.

Naye Mkuu wa Shule ya Polisi Moshi SACP Ramadhan Mungi, amesema kuwa, jumla ya wahitimu 2030 wamehitimu mafunzo ya miezi minne na kupandishwa Cheo cha Mkaguzi Msaidizi wa Polisi ambapo kwenye mafunzo hayo askari wamepata maarifa na ujuzi wa kutosha katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu

Post a Comment

0 Comments