Ticker

6/recent/ticker-posts

MRADI WA KUPUNGUZA UMASIKINI AWAMU YA NNE WAACHA TABASAMU KWA WANANCHI

Na Said Mwishehe,Michuzi TV -Karatu

MKURUGENZI Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) Shedrack Mziray ametoa taarifa ya mafanikio ya Mradi wa Kupunguza Umaskini awamu ya Nne (TPRP IV) ambao umekuwa mradi mahiri na wa kimkakati uliotekelezwa na Mfuko huo.

Akizungumza na Waandishi wa habari wilayani Karatu mkoani Arusha kuhusu mradi huo ambao umefika tamati Mziray amesema umechangia kwa kiwango kikubwa kuendeleza ajenda yao ya maendeleo ya taifa, hususan kupunguza umaskini, kuboresha huduma za kijamii, na kuwezesha jamii kote nchini Tanzania.

“Tangu kuanza kwa mradi huu Januari 2020, TPRP IV umejikita kimkakati katika kupunguza umaskini katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Njombe, Geita na Simiyu.

“Lengo kuu lilikuwa ni kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii na fursa za kuongeza kipato, hii imefanyika kwa kupitia ujenzi na ukarabati wa miundombinu lengwa, mradi umewezesha ujenzi na ukarabati wa madarasa, vituo vya afya na vyanzo vya maji ambavyo sasa vinahudumia kaya za walengwa pamoja na jamii kwa ujumla.

“Uwekezaji huu umeongeza upatikanaji wa huduma, umepunguza umbali wa kufikia huduma za afya na maji, na kuimarisha mazingira wezeshi kwa ustawi wa jamii.

Mradi pia umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha ustahimilivu wa kiuchumi.”

Pia Kaya zilisaidiwa kutanua wigo wa vyanzo vya kipato kupitia shughuli kama ajira binafsi katika sekta mbalimbali ikiwemo za kilimo, ufugaji wa mifugo na shughuli nyingine za uzalishaji.

Amefafanua matokeo yake, familia nyingi zimeongeza kipato cha kaya, kuboresha usalama wa chakula na kuimarisha uwezo wa kukidhi mahitaji ya msingi.

“Tathmini za hivi karibuni zinaonesha kuwa mradi huu (TPRP IV) umenufaisha kaya takriban 200,007 kwa kiwango cha mwitikio wa asilimia 96.7, jambo linaloonesha wigo mpana na athari chanya za afua za mradi.

“Mojawapo ya mafanikio makubwa ni kukuza usawa wa kijinsia na kuunga mkono elimu ya wasichana. Ujenzi wa mabweni, vyoo na madarasa umeongeza uandikishaji, kuboresha udumishaji wa wanafunzi shuleni, na kupunguza mimba za utotoni.”

Mziray amesema hatua hizo zimechangia kuboresha matokeo ya kielimu na kuongeza fursa kwa wasichana. Msisitizo wa ushirikishwaji wa jamii umejenga uwajibikaji wa pamoja na uendelevu, kuhakikisha rasilimali zinaendelea kufanya kazi na kutunzwa hata baada ya mradi kukamilika.

Pia amesema ushiriki wa wanawake umekuwa nguzo ya mafanikio huku akisisitiza asilimia 56.5 ya kaya nufaika za Mradi huu zinaongozwa na wanawake ambapo wanashiriki kikamilifu katika usimamizi wa miradi, akiba na uongozi.

Amesema itihada za kuongeza kipato cha kaya zimeleta matokeo chanya, huku kaya nyingi zikiongeza kipato na kudizi Sh.200,000 wakati wa utekelezaji.

Ameongeza vikundi vya akiba na shughuli za mikopo vimeziwezesha jamii, ambapo asilimia 88.3 ya kaya zina uelewa wa mifumo ya akiba na asilimia 38.9 zimepata ongezeko la upatikanaji wa mikopo, hivyo kuimarisha ustahimilivu wa kiuchumi na uhuru wa kifedha.

Pia mafunzo ya ujasiriamali yamewafikia asilimia 82.4 ya kaya, yakichochea biashara mpya na kuongeza vyanzo vya kipato, hususan miongoni mwa wanawake wanaochukua nafasi za uongozi na kuanzisha shughuli endelevu za uzalishaji.

“Mafanikio ya TPRP IV yamejengwa kupitia dhamira thabiti ya kisiasa katika ngazi za kitaifa na za serikali za mitaa, ushiriki madhubuti wa jamii, na uratibu mzuri wa wadau. Mamlaka za serikali za mitaa zinaendelea kusimamia uendeshwaji na matumizi ya miradi iliyotekelezwa.”

Amesema wanaposherekea mafanikio haya, pia wanatambua changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji, ikiwemo ucheleweshaji wa malipo na mahitaji ambayo hayakukidhiwa kikamilifu katika miundombinu ya maji na afya.

“Changamoto hizo zimetupatia masomo muhimu kwa siku zijazo. Tumejipanga kuzishughulikia kupitia ujenzi wa uwezo, kuimarisha ushirikiano, kuboresha mipango, na afua lengwa hususani katika kuendeleza uwezo katika ngazi ya PAA na kurahisisha michakato ya usajili wa vikundi vya akiba ili kudumisha mafanikio na kupanua athari.”

Post a Comment

0 Comments