Ticker

6/recent/ticker-posts

KCB YANUFAISHA VIJANA 304 ELIMU UJASIRIAMALI

Mkuu wa masoko, Uhusiano na Mawasiliano wa KCB, Christina Manyenye


TAKRIBAN vijana 304 katika Mikoa mbalimbali nchini, wameondokana na dhana ya kusubiri kuajiriwa baada ya kunufaika na elimu ya ujasiriamali na hivyo kujiajiri. 

Hatua hiyo ni baada ya kupata mafunzo hayo kupitia Programu ya 'Vijana Tujiajiri' iliyoanzishwa na Benki ya KCB nchini. 

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkuu wa masoko, Uhusiano na Mawasiliano wa Benki hiyo, Christina Manyenye, alisema shabaha ya kuanzisha programu hiyo ni kufungua fursa kwa vijana. 

Alibainisha katika vijana hao 304 wanawake ni 256, waliopita mafunzo hayo katika Vyuo mbalimbali vya Ufundi Stadi (VETA). 

Mbali na vijana hao, alieleza Oktoba 18, mwaka huu wengine 200 wanatarajiwa kuanza masomo ili kunufaika na programu hiyo, huku lengo likiwa ni kuwafikia vijana 4,000 nchini. 
 
"Ukiangalia tangu tumeanza programu hii mwaka 2016 wanawake 256 wamenufaika na mafunzo darasani na vitendo," alisema. 

Alifafanua kupitia programu hiyo, vijana wanafundishwa ujasiriamali, namna ya kutunza kumbukumbu za fedha na biashara zao, kadhalika mbinu za kutafuta masoko. 

"Katika hawa pia wapo wanawake walionufaika na ruzuku ya sh. milioni tano kwa kila mmoja ili kuendeleza biashara zao," alisema Christina.
 
Aidha, alieleza kwa sasa programu hiyo inafanyika katika maeneo mbalimbali nchini vikiwemo visiwa vya Zanzibar, Morogoro, Arusha, Dar es salaam, Mwanza na Moshi. 
 
Kuhusu mchango wa Benki hiyo kwa serikali, Christina aliweka wazi kwamba tangu kuanzishwa kwake imetoa takribani sh. bilioni 63 ikiwa ni kodi kwa serikali. 
 
"Benki ya KCB imekuwa na mwenendo mzuri wa ulipaji kodi ambapo kwa mwaka inakadiriwa kulipa kodi ya sh. bilioni 13," alieleza. 

Post a Comment

0 Comments