Ticker

6/recent/ticker-posts

WAKULIMA MIWA WAPEWA MBINU BORA ZA UZALISHAJI

WATAALAMU wa Mawasiliano na Utafiti  wa Taasisi ya Utafiti  wa Kilimo (TARI)- Kibaha na Maofisa Ugani wa Wilaya ya Kilosa wakiakagua maandalizi ya shamba la miwa kabla ya upandaji wilayani humo.

NA MWANDISHI WETU

WAKULIMA wa zao la miwa wameshauriwa kufuata maelekezo mbalimbali ya wataalamu wa kilimo ili kuongeza uzalishaji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta hiyo nchini.

Ushauri huo ulitolewa na wataalamu mbalimbali wa kilimo kutoka Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, walipozungumza nna wakulima katika vijiji vinavyozalisha miwa ndani ya wilaya hiyo.

Devotha Mng’andile ni Ofisa Ugani wa Kijiji cha Kifinga kata ya Ruaha, alisema iwapo wakulima watazingatia utaalamu unaotolewa katika uzalishaji wa miwa mnyororo wa  thamani wa zao hilo utaongezeka na hivyo kipato kukua.

“Tunachojivunia ni kuona sisi maofisa Ugani tuliopo vijijini tunawezeshwa kiutalaamu na wenzetu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI)-Kibaha na hivyo tumekuwa na uwezo mkubwa wa kuwafikishia wakulima maarifa mapya.

“tunachowaomba wakulima ni kuyafanyia kazi maarifa hayo”, alisema.

Alieleza wataalamu kutoka TARI- Kibaha wamewajengea uwezo wa kutosha wa kufahamu namna bora ya kuwahudumia wakulima wa miwa wilayani humo, tayari wameanza kuona mafanikio katika uzalishaji.

Kwa upande wake, Ofisa Kilimo wa kijiji cha Lwemba, Kata ya Kidodi, Sarah Wolter, alisema kwa sasa pamoja na kutoa elimu kwa wakulima wa zamani, pia wameanza mchakato wa kutoa elimu kwa vijana ili washiriki katika kilimo cha miwa.

“Kilimo cha miwa kinalipa sana na unaweza kujikuta unaingiza fedha za kutosha ikiwa unalima kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa kilimo, ndiyo maana sisi kama wataalamu tumekuwa tukishirikiana bega kwa bega na wananchi katika kufanikisha kilimo bora”, alisema.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Kidodi AMCOS, Onesmo Mwakyambo, alisema kwa kushirikiana  na maofisa Ugani na wataalamu kutoka  TARI-Kibaha  wanachama wake wamefaidika.

Alisema wamepata utaalamu wa uzalishaji wa miwa kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi na matumizi ya sayansi na teknolojia.


Post a Comment

0 Comments