Ticker

6/recent/ticker-posts

WATALII WATEMBEKELEA HIFADHI YA TAIFA NYERERE SIKU YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE


Watalii mbalimbali wakiwasili katika uwanja wa Mtemere kwaajili ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Nyerere iliyopo wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani. Mhifadhi Mwandamizi Bw.Seti Mihayo akizungumza na baadhi ya wanafunzi waliofika kwaajili ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Nyerere katika geti la Mtemere kwenye Hifadhi ya Taifa Nyerere iliyopo wilayani Rufiji mkoa wa Pwani.Mhifadhi Mwandamizi Bw.Seti Mihayo akizungumza na waandishi wa habari katika geti la Mtemere katika Hifadhi ya Taifa Nyerere iliyopo wilayani Rufiji mkoa wa Pwani. 

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO) 

******************* 

NA EMMANUEL MBATILO, RUFIJI 

Tukiwa tunaadhimisha Kumbukumbu ya kifo cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere kila ifikapo Oktoba 14 kila mwaka, Watalii mbalimbali wametembelea Hifadhi ya Taifa Nyerere kwaajili ya kuona vivutio na kumuenzi Mwalimu Nyerere. 

Akizungumza katika hifadhi hiyo Mhifadhi Mwandamizi, Bw.Seti Mihayo amesema hifadhi hiyo ni kubwa barani Afrika na inawanyama wa aina mbalimbali ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa ni vivutio kwa wageni. 

"Hifadhi hii ni ya kipekee sana kwasababu inavivutio tofauti tofauti ikiwemo wanyama adimu kama Mbwa mwitu,Viboko,Simba,Chui,Twiga,Nyati na wanyama wengine wengi wanapatikana hapa". Amesema Bw.Seti. 

Ameongeza "Hifadhi ina ukubwa wa kilometa 30893 ambayo ilitengwa kutoka katika pori la akiba la Selou kwamaana kwamba ni Hifadhi kubwa Afrika na ina Mito kama Rufiji ambao ni Mkubwa na Mto Kilombero". 

Alisema hifadhi hiyo iko karibu na Mkoa wa Dar es Salaam ambapo ni takribani kilometa 190 huku kwa mkoa wa Morogoro ikiwa ni kilometa 162. 

Alisema miongoni mwa kivutio kingine ambacho kipo ndani ya hifadhi hiyo ni mti wa maajabu ambao uligoma kung'olewa ili kupisha ujenzi wa barabara. 

"Mti huo zamani ulitumika kwa matambiko kwani wakati huo ndani ya hifadhi hii kulikuwa na vijiji ambavyo waliutumia na baada ya kujaribu kuung'oa imeshindikana kutokana na vifaa kuharibika hivyo tumeamua kuuacha ili kuwa sehemu ya kivutio,"alibainisha 

Seti ametoa wito kwa Watanzania kutembelea hifadhi hiyo ili kujionea vivutio hivyo vya wanyama na kihistoria. 

Miongoni mwa makundi yaliyotembelea hifadhi hiyo ni Tanzania Land rover Club kutoka Dar es Salaam na Morogoro. 

Mratibu wa kikundi hicho Bw.Meja Mbuya amesema wameamua kutembelea sehemu hiyo ili kuhamasisha utalii wa ndani katika hifadhi hiyo. 

"Tumetumia usafiri wa Landrover kwasababu baba wa Taifa alitumia aina hii ya gari katika harakati za ukombozi wa nchi na pia viongozi wengi wa Afrika wametumia katika kupigania uhuru wa bara la Afrika". Amesema. 

Kwa upande wako mmoja wa watalii wa ndani, Maria Wilson alisema amekuja kutembelea hifadhi hivyo ikiwa ni sehemu ya kumkumbuka Hayati Nyerere. 

"Ninaamini kuwa nitaona mengi na nitajifunza vitu vingi kupitia hifadhi hii na pia nimekuja na wanafunzi zaidi ya 100 wa shule ya msingi Mloka na wao watajifunza kuhusu baba wa taifa na wataona wanyama mbalimbali". Amesema 

Naye mmoja wa wanafunzi waliotembelea hifadhi hiyo, Mustakim Kingwande, alisema anamfahamu baba wa Taifa kwa kumsoma katika vitabu vya histori hivyo fursa ya kutembelea hifadhi ni nafasi nzuri ya kujifunza. 

"Nimekuwa nikiendelea kujifunza kuhusu mwalimu Nyerere na nilitamani kutembelea hifadhi yake ili kujifunza nimefanikiwa nafurahi kwa hili,"alieleza.

Post a Comment

0 Comments