Ticker

6/recent/ticker-posts

WILAYA YA TEMEKE KUANZISHA GULIO LA WAFANYABIASHARA NA WAMACHINGA



Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam Jokate Mwegelo(kulia) akizungumza na waandishi wa habari leo oktoba 13,2021 alipokuwa akitangaza kuanza kwa Temeke Gulio ikiwa ni mkakati wa kuweka mazingira ya wafanyabiashara kufanya biashara katika maeneo rasmi.Kushoto ni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Temeke. 

Baadhi ya wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo Jokate Mwegelo(hayuko pichani) wakati akitangaza Temeke Gulio leo Oktoba 13,2021. 

****************** 

Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imetangaza kuanzisha Gulio ili kuwakusanya wafanyabiashara hasa wamachinga wilayani humo kufanya biashara kwa utaratibu maalum. 

Akizungumza na waandishi wa Habari jana Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe.Jokate Mwegelo amesema Temeke Gulio itakuwa njia mojawapo kuwaondoa wafanyabiashara waliokaa maeneo yasiyoruhusiwa na kupelekwa maeneo ambayo wanastahili kufanyabiashara. 

"Ifikapo Octoba 18,2021 tutatamani kuona Machinga wakiwa katika maeneo ambayo yanaruhusiwa, Temeke tunawapenda wafanyabiashara wetu,hivyo tumekuja na Temeke Gulio kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara,"amesema DC Jokate. 

Amefafanua kuwa Manispaa ya Temeke imeshaweka utaratibu mzuri kwa ajili ya wafanyabiashara."Manispaa ya Temeke imejenga masoko mengi chini ya Mradi wa Kuendeleza Jiji la Dar es Salaam (DMDP), ambayo yalikuwa hayafanyi vizuri hivyo baadhi ya wafanyabiashara watakwenda kufanyabiashara zako huko. 

"Kwanza nawapongeza sana ndugu viongozi wa Wamachinga Temeke kwani tunashirikiana vizuri, hivyo basi tuna maeneo 20 yaliyotengwa kwa ajili yenu, namshukuru Mkurugenzi wa Manispaa, Elihuruma Mabelya kwa kazi kubwa aliyoifanya katika hili,"amesema Jokate. 

Pia amesema kuwa maeneo mengine ambayo yametengwa kwa ajili ya wafanyabiashara ni Buza Makangarawe, Mbagala, Zakhem na Vetenari pamoja maeneo mengine ambapo tayari wao kama viongozi wameshatoa maelekezo na elimu kuhusu mchakato huo. 

Hivyo amesisitiza katika kuboresha mazingira ya biashara wameamua kuzindua Kampeni ya Temeke Gulio ,lengo ni kufungua fursa za kibiashara na wafanyabiashara kushiriki kilamilifu katika kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia biashara wanazofanya. 

"Wafanyabiashara niwaambie tu Temeke Gulio inakwenda kutoa fursa kwenu, tunatarajia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam atazindua rasmi,"amesema Jokate na kusisitiza hadi hivi sasa wamewatambua wafanyabishara 5,875 na kati ya hayo 1600 wameomba nafasi na nafasi zilizobaki ni 3,000. 

Katika hatua nyingine, Jokate amempongeza Rais Samia Suluhu kwa kuipatia Wilaya ya Temeke Sh.bilioni tano kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali iliyopo ndani ya wilaya hiyo ikiwamo kutatua changamoto ya madawati na madarasa ambapo mwaka ujao wanafunzi wote wa kidato cha kwaza wataingia kwa awamu moja. 

"Fedha zingine zitakwenda kujenga Kituo cha Afya Mbagala, Tuangoma na zingine zitakwenda kujenga majengo ya huduma za dharura, pia kujenga bweni la Shule ya Sekondari Kibasila na nyingine zitakwenda kwenye mapambano dhidi ya Uvid-19.Hapa nisemme tu tunamshukuru sana Rais wetu kwa upendo wake mkubwa kwetu,kweli hadi ifikapo 2025 atakuwa amefanya mambo makubwa ya maendeleo kwa ajili ya Watanzani,"amesema. 

Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya hiyo, Daniel Sayi ameeleza kufufahishwa na kampeni ya Temeke Gulio iliyoanzishwa na wilaya hiyo chini ya Mkuu wa Wilaya Jokate."Yote yanayofanyika ni utekelezaji wa Ilani ya Chama. 

"Hivyo wajibu wetu ni kuhakikisha tunasimamia kuona ahadi zote zinatekelezwa,lengo ni kuboresha maisha ya wananchi ,kutatua changamoto na kuleta maendeleo ,"amesema. 

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke Mabelya amemuwahakikishia Mkuu wa Wilaya hiyo fedha ambazo zinatolewa na Rais Samia kwa Wilaya hiyo hakuna hata senti moja itakayotumika kinyume na makusudio ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Post a Comment

0 Comments