Ticker

6/recent/ticker-posts

WATU WAWILI WAKAMATWA NA POLISI WAKIWA NA VIPANDE SABA VYA MENO YA TEMBO MKOANI MBEYA



**************************

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili 1. LIPANDE SAID @ SIMWICHE [62] na 2. JUMA PIUS [32] wote wakazi wa Kapyo wilayani Mbarali mkoani Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali vipande saba [07] vya Meno ya Tembo.

Watuhumiwa walikamatwa tarehe Oktoba 20, 2021 majira ya saa 10:00 asubuhi huko Kijiji cha Kapyo kilichopo Kata ya Igurusi, Tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali baada ya Jeshi la Polisi mkoani hapa kupata taarifa za siri na kisha kufanya msako na upekuzi nyumbani kwa mtuhumiwa LIPANDE SAID @ SIMWICHE na kufanikiwa kukuta nyara hizo zikiwa zimefichwa kwenye mfuko wa sandarusi.

Aidha katika upekuzi huo, watuhumiwa walikutwa wakiwa na nyara nyingine za serikali ambazo ni kipande cha Ngozi ya Fisi Maji nacho kikiwa kimefichwa kwenye mfuko wa sandarusi.

Vipande hivyo saba vya Meno ya Tembo vina uzito wa kilogramu 33 na thamani ya Tshs. Milioni Sitini na tisa laki mbili kumi na nne elfu mia nne na kumi [Tshs.69,214,410/=] huku ikikadiriwa kuwa Tembo waliouawa ni wawili.

Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa kosa la kupatikana na nyara za serikali kinyume cha sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009 kifungu namba 86 na kosa la uhujumu uchumi kinyume cha sheria ya uhujumu uchumi ya mwaka 2019 kifungu namba 57 (First Schedule).

ATAFUTWA NA JESHI LA POLISI KWA KOSA LA KUTUPA MTOTO.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamtafuta mwanamke ambaye bado hajafahamika kwa kosa la kutupa mtoto mchanga jinsi ya kike anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya siku tatu ambaye alikutwa amefariki dunia baada ya kutupwa ndani ya shimo la choo.

Tukio hilo limetokea mnamo Oktoba 20, 2021 majira ya saa 09:00 asubuhi huko Mtaa wa Makaburini uliopo Kata ya Kiwira, Tarafa ya Ukukwe katika Halmashauri ya Tukuyu. Mwili wa kachanga ulikutwa ndani ya shimo la choo kilichopo nyumbani kwa SALOME LUTENGANO [36] Mkazi wa Mtaa wa Makaburini na ndipo jitihada za kuutoa zilianza lakini tayari alikuwa amefariki dunia.

Jeshi la Polisi Mkoani hapa linalaani kitendo hicho cha mauaji ya mtoto asiyekuwa na hatia yoyote na linaendelea na msako dhidi ya mtuhumiwa wa tukio hili na mara baada ya kumkamata litamfikisha mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.


MWANAFUNZI WA KIDATO CHA TATU AFARIKI DUNIA BAADA YA KUANGUKA CHOONI.

Mwanafunzi wa kidato cha tatu FRANCIS MWAKAJOKA [16] wa shule ya sekondari Wigamba iliyopo Jijini Mbeya amefariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa matibabu baada ya kuanguka kwenye Koldo la choo shuleni hapo.

Tukio hilo limetokea Oktoba 20, 2021 majira ya saa 07:45 asubuhi huko Shule ya sekondari Wigamba iliyopo Jijini Mbeya. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kitabibu. Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa marehemu alikuwa na matatizo kwenye mapafu.

Post a Comment

0 Comments