Ticker

6/recent/ticker-posts

WIZARA YAONGEZA NGUVU KUDHIBITI UTOROSHAJI MAZAO YA UVUVI

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Bw. Emmanuel Bulayi (kushoto), akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah (katikati) juu ya utendaji kazi wa injini tano za kupachika kwenye boti zilizonunuliwa na idara hiyo kwa ajili ya vituo vya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi Kanda ya Ziwa Victoria. Hafla hiyo fupi imefanyika katika ofisi za wizara hiyo zilizopo Mtumba jijini Dodoma. Aliye upande wa kushoto kwa katibu mkuu ni Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbemaji Dkt. Nazael Madalla. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) akimkabidhi injini ya kupachika kwenye boti Afisa Mfawidhi Kituo cha Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Kanda ya Mwanza Bw. Gabriel Mageni na kuwataka maafisa wafawidhi kuhakikisha wanatumia vifaa hivyo kwa ajili ya kudhibiti utoroshaji wa mazao ya uvuvi kwenda nchi za jirani, kukusanyia maduhuli na kuzuia uvuvi haramu. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah (mwenye suti nyeusi), akiwa kwenye zoezi la kukabidhi injini za kupachika kwenye boti kwa maafisa wafawidhi wa vituo vya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi Kanda ya Ziwa Victoria. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah, akiwa kwenye picha ya pamoja na watendaji wakuu wa idara mbalimbali katika Sekta ya Uvuvi wizarani hapo, pamoja na maafisa wafawidhi wa vituo vitano vya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi Kanda ya Ziwa Victoria. Dkt. Tamatamah amekabidhi injini tano za kupachika kwenye boti katika vituo hivyo zenye thamani ya jumla ya Shilingi Mlioni 68.1 (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).


*******************************


Na. Edward Kondela


Serikali imewataka maafisa wafawidhi waliopo katika vituo vya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi Kanda ya Ziwa Victoria, kuhakikisha wanadhibiti utoroshaji wa mazao ya uvuvi kwenda nchi za jirani pamoja na kuzuia uvuvi haramu.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema hayo leo (28.10.2021) katika ofisi za wizara hiyo zilizopo Mtumba jijini Dodoma, wakati akikabidhi injini za kupachika kwenye boti zenye uwezo “HP 40” kwa vituo vitano vya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi Kanda ya Ziwa Victoria.

“Ni matumaini yangu kuwa injini hizi zitakuwa chachu kwa vituo hivi kufanya kazi kwa weledi pamoja na kusimamia ulinzi wa rasilimali za uvuvi.” Amesema Dkt. Tamatamah
Aidha, amesema ili kufikia malengo ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya kukusanya maduhuli ya Shilingi Bilioni 40 kwa mwaka wa fedha 2021/22, injini hizo zitumike katika kuhakikisha vituo husika vinakusanya maduhuli ili kufikia malengo waliyojiwekea na kufikia malengo makuu ya wizara.

Nao baadhi ya maafisa wafawidhi waliokabidhiwa injini za boti kwa ajili ya vituo vyao vya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi wamesema injini hizo zitasaidia kuongeza nguvu katika kudhibiti uvuvi haramu.

Wameongeza pia injini hizo zitasaidia katika kufuatilia ukusanyaji wa mapato ambayo ni moja ya mikakati ya wizara na kudhibiti utoroshaji wa mazao ya uvuvi kwenda nchi za jirani.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Idara ya Uvuvi imenunua injini sita za kupachika kwenye boti zenye thamani ya Shilingi Milioni 68.1 kwa ajili ya kuimarisha Sekta ya Uvuvi nchini.

Vituo vitano vya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi vilivyokabidhiwa injini hizo ni Kanda ya Simiyu na Magu, Kanda ya Mwanza, Kanda ya Ukerewe, Kanda ya Geita na Kanda ya Marehe Mkoani Kagera.

Post a Comment

0 Comments