Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUONDOA ZUIO LA BIASHARA YA USAFIRISHAJI WANYAMAPORI HAI NJE YA NCHI


*****************************

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema Serikali itaondoa zuio la biashara ya usafirishaji wa wanyamapori hai nje ya nchi lakini wafanyabiashara watatakiwa kuzingatia taratibu za usafirishaji.

Ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Eng. Mwanaisha Ulenge aliyehoji lini Serikali itaruhusu usafirishaji wa viumbe hai nje ya nchi.

Mhe. Masanja amefafanua kuwa baada ya Serikali kutathmini kuhusu usafirishaji wa wanyamapori hai nje ya nchi imekubali kuondoa zuio hilo kwa masharti kwamba wanyamapori hai wasafirishwe kwa shughuli za utafiti na kidiplomasia tu; wawe wamekaushwa au ni mazao yatokanayo na wanyamapori na kwamba wasafirishaji hao ni lazima wawe ni wafanyabiashara wenye miradi ya ufugaji wanyamapori ili kuhamasisha uanzishwaji wa miradi ya ufugaji wa wanyamapori.

Aidha, Serikali itatoa muda wa miezi mitatu kuruhusu wafanyabiashara kusafirisha wanyamapori waliosalia kwenye mazizi na mashamba kabla ya zuio ambao walikuwa wanafugwa kwa lengo la kuwasafirisha nje ya nchi.

Serikali ilisitisha biashara ya kusafirisha wanyamapori nje ya nchi tartehe 17/03/2016 baada ya kuonyesha matokeo hasi ya biashara ikiwa ni pamoja na uhamishaji warasilimali za wanyamapori nje ya nchi.

Post a Comment

0 Comments