Ticker

6/recent/ticker-posts

MAJALIWA AIPONGEZA SEKTA BINAFSI KWA KUKUZA SEKTA YA AJIRA NCHINI


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Mkutano wa Mwaka wa CEO Roundtable of Tanzania akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Hoteli ya Hayatt Regency mkoani Dar es salaam, Desemba 4, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Mwaka wa CEO Roundtable of Tanzania wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Hoteli ya Hayatt Regency mkoani Dar es salaam, Desemba 4, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Mwaka wa CEO Roundtable of Tanzania baada ya kuzungumza akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Hoteli ya Hayatt Regency mkoani Dar es salaam, Desemba 4, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

***************************

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameipongeza sekta binafsi kwa namna inavyoshiriki katika kukuza uchumi wa nchi ikiwemo kutoa fursa za ajira kwa watanzania kupitia makampuni na mashirika mbalimbali nchini.

Amesema kuwa moja ya mafanikio makubwa ni kuongezeka kwa ajira milioni 3.6 kutoka ajira milioni 20.5 mwaka 2014 hadi ajira milioni 24.1 mwaka 2020/2021 na kuongezeka kwa ajira kwenye sekta isiyo rasmi kutoka asilimia 22.0 mwaka 2014 hadi asilimia 29.4 mwaka 2020/2021.

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Jumamosi Disemba 5, 2021) Alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Jumuia ya Watendaji Wakuu wa Makampuni na Mashirika (CEO Roundtable of Tanzania) katika ukumbi wa hoteli ya Hyatt Regency, Mkoani Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema licha ya changamoto ya UVIKO 19, Tanzania imeendelea kufanya vizuri kwenye sekta nyingine za kiuchumi na kutoa ajira katika sekta ya kilimo hivyo kutoa mwelekeo mzuri katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano inayolenga kuwa na asilimia 60 ya ajira kwenye kilimo ifikapo mwaka 2025/2026.

“Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti ya kuimarisha uwekezaji, biashara na kuongeza wigo wa vyanzo vya mapato kwa kushirikiana na sekta binafsi. Hatua hizo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa uwekezaji nchini hususan kutoka nje ambao kwa mwezi Machi hadi Agosti 2021 ulifikia takriban Dola za Marekani bilioni 3.00.”

Waziri Mkuu amesema Rais Samia ameendelea kuimarisha mazingira bora ya uwekezaji na ufanyaji wa biashara na anaamini kupitia mkutano huo wataweza kutoa ushauri na mapendekezo ya namna bora ya kuimarisha shughuli za biashara na uwekezaji.

Aliongeza kuwa Serikali ina matarajio na sekta binafsi kuwa itaendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika kupambana na kupunguza hewa ya ukaa na matumizi ya Plastiki. “Ongezeni uwekezaji kwenye miradi ya matumizi ya nishati mbadala, Ustawishaji wa misitu na utunzaji wa mazingira na usafirishaji kwa kutumia teknolojia za kisasa zisizozalisha hewa ya ukaa”

“Nitoe wito kwenu kuendelea kuwaita wawekezaji, kuja hapa nchini na kuwekeza katika Sekta mbalimbali za kilimo, utalii na nishati”

Naye, Mwenyekiti wa “CEO Roundtable of Tanzania” Bw. Sanjay Rughani ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa namna inavyoshirikiana na sekta binafsi katika kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara na watahakikisha kupitia shughuli zao wataifanya Tanzania kukua kiuchumi sio tu Afrika bali duniani kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments