Ticker

6/recent/ticker-posts

MAWAZIRI WA AFYA KUTOKA NCHI ZA EAC WAKUTANA MJINI ZANZIBAR

Mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta (BLM) la Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umefanyika tarehe 10 Desemba 2021 katika Hotel Verde mjini Zanzibar.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri ulitanguliwa na mikutano miwili ya awali iliyofanyika tarehe 6 hadi 8 Desemba 2021na tarehe 9 Desemba 2021 katika ngazi ya Wataalamu na Makatibu Wakuu mtawalia.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (Mb) aliwakaribisha wajumbe wa mkutano huo mjini Zanzibar na kupongeza maamuzi yaliyofikiwa na sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya kwamba mkutano huo ufanyike mjini humo ili kuwapa fursa wajumbewa mkuano huo kuyafahamu maeneo ya utalii ndani ya kanda.

Vilevile alieleza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kufanyia kazi maamuzi na mapendekezo mbalimbali yanayotolewa na vikao hivyo ili yaweze kuwa na tija kwa masalahi ya wananchi ndani ya jumuiya.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Sekta ya Uzalishaji na Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo katika ufunguzi wa mkutano huo aliipongeza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mapokezi mazuri kwa wajumbe wa mkutano huo na kwa kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kupongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kurasimisha lugha nyingine zitakazotumiwa katika mikutano ya jumuiya hiyo ambapo, alieleza mpaka sasa Sekretarieti ya Jumuiya hiyo inafanyia kazi taratibu za kuifanya lugha za Kiswahili na kifaransa kuwa lugha rasmi kwa ajili ya matumizi ya mikutano ya jumuiya.

Pia akapongeza juhudi zilizooneshwa na Shirika la

Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kuifanya tarehe 7 Julai kuwa siku ya Kiswahili.

“UNESCO imeonesha ni namna gani lugha ya Kiswahili ambayo ndio lugha pekee ya kiafrika yenye watumiaji wengi imeweza kuthaminiwa ulimwenguni, sisi kama jumuiya tutaendeleza jitihada za kukuza Kiswahili” alisema Mhe. Bazivamo.

Kadhalika, Mhe. Bazivamo amezisisitiza Nchi wanachama wa jumuiya hiyo kukamilisha zoezi la uandaaji wa Hati za Kusafiria za Kielekronik za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC e-Passport) ambapo, ameeleza mpaka sasa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pekee ndio imefanikiwa kukamilisha zoezi la ugawaji wa Hati hizo za kusafiria kwa wananchi wake.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (Mb.) Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambaye ameambatana na Mhe. Dkt. Godwin Mollel (Mb.) Naibu Waziri, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Tanzania Bara.

Viongozi wengine walioshirikia mkutano huo ni pamoja na; Dkt. Fatma H. Mrisho, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; Dkt. Othman Mohamed Ahmed, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia - Tanzania Bara, Bw. Eliabi Chodota, Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; na Dkt. Abdul S. Ali, Mganga Mkuu na Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Pamoja na mambo mengine Mkutano

wa 21wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la

Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umepokea

taarifa ya utekelezaj wa maamuzi/maagizo ya

mikutano iliyopita; hali ya mlipuko wa janga la

UVIKO -19 Kikanda; na Utekezaji wa programu

na miradi ya Afya.


Mkutano huu umehudhuriwa

 na nchi zote wanachama isipokuwa Jamhuri ya


Rwanda na Jamhuri ya Sudani Kusini ambao


walishiriki mkutano kwa njia ya mtandao.




==============================



Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Godwin Mollel (Mb) akifafanua jambo wakati wa Mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 10 Desemba 2021 katika Hotel Verde mjini Zanzibar. Pembeni yake ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui.


Meza kuu wakiongozwa na Mwenyekiti wa mkutano huo Naibu Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Rashid Aman (wa pili kutoka kulia). Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Sekta ya Uzalishaji na Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo.


Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota pamoja na Mganga Mkuu na Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Abdul S. Ali wakifuatilia mkutano.


Ujumbe wa Tanzania


Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania


Ujumbe kutoka Burundi


Ujumbe kutoka Uganda


Picha ya pamoja viongozi wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mawaziri wa Afya wa Jumuiya hiyo walioshiriki mkutano.



Mkutano ukiendelea

Post a Comment

0 Comments